Maswali kutekwa mwanafunzi, kuuawa na mwili kuchomwa

Mbeya. Aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe ndaki ya Mbeya, Shairose Mabula ameuawa kikatili kisha mwili kuchomwa moto, tukio lililoibua simanzi na maswali lukuki.

Mwili wa mwanafunzi huyo ukitarajiwa kuzikwa kesho Jumamosi, Septemba 20, 2025, baba yake mzazi, Dk Mabula Mahande, amesimulia tukio hilo huku akiliomba Jeshi la Polisi kuongeza nguvu kuwabaini na kuwakamata waliohusika.

Kwa mujibu wa Dk Mahande, kabla ya tukio hilo aliwahi kumtahadharisha mwanaye kuwa makini kutokana na vitendo vya utekaji na mauaji.

Dk Mabula aliyetia nia kuwania ubunge Mbeya Mjini, amelieleza Mwananchi kuwa wiki moja nyuma, mfanyakazi wake wa dukani alinusurika kutekwa katika eneo la Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Alitia nia kuwania ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na katika kura za maoni alishika nafasi ya pili kwa kura 1,133 nyuma ya Patrick Mwalunenge aliyepata kura 3,360, ambaye anapeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Shairose aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Kitivo cha Sheria anadaiwa kutekwa, kuuawa na mwili kuchomwa moto katika Mtaa wa Moravian, Kata ya Isyesye, jijini Mbeya.

Alitoweka nyumbani kwao Mtaa wa Uzunguni takribani siku tatu kabla ya jana Septemba 18, kusambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kifo chake.

Dk Mabula akiwa nyumbani kwake Mtaa wa Uzunguni leo Septemba 19, amesema chanzo cha kifo cha mwanaye huyo wa kwanza, bado hakijafahamika, akieleza katika shughuli zake hajawahi kuwa na mgogoro ama wa kibiashara au kisiasa.

Kutokana na tukio hilo, amesema anaviachia vyombo vya usalama kuendelea kulishughulikia, kwani mwanaye hakuwahi kumweleza iwapo ana mtu anamsumbua kwa namna yoyote.

“Hili ni tukio la kwanza kwa familia na ukoo wangu, ila kuna jaribio la utekaji liliwahi kumtokea mfanyakazi wangu, wakataka kumbeba kwenye gari. Sielewi kilichopo nyuma, ila kwa kuwa uchunguzi unaendelea ninasubiri,” amesema na kuongeza:

“Tunatarajia kuzika kesho hapa Mbeya mjini, lakini niombe Serikali uchunguzi ufanyike, waliohusika wakamatwe. Jeshi la Polisi liongezewe vifaa vya kisasa kwa kuwa teknolojia inabadilika ili kusaidia ufanisi wa kazi zao.”

Amesema kabla ya kupokea taarifa za kifo, waliohusika walimpigia simu kwa kutumia simu ya mwanaye, wakieleza kumshikilia na wanakwenda naye Tabora, huku wakihitaji fedha (hakutaja kiasi). Amesema namba aliyotakiwa kutuma fedha hizo ilikuwa tofauti, iliyosomeka wilayani Chunya.

Dk Mabula amesema pia alitumiwa video ikionyesha namna mwanaye anavyoteswa kupitia namba yake ya simu, ushahidi anaosema ameuwasilisha polisi.

“Watekaji walikuwa wakijinasibu hakuna anayewaweza kwa kuwa wana uwezo hata kuzidi Jeshi la Polisi, kwa maana hiyo naamini wana uzoefu kwenye hili na walijiandaa,” amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, katika taarifa iliyotolewa Septemba 18, alisema Septemba 14, 2025 Mabula alifika kituo kikuu cha Polisi Mbeya kutoa taarifa ya kupotea kwa binti yake.

Baada ya taarifa hiyo lilifungua jalada la uchunguzi na ufuatiliaji ili kumpata. Septemba 16, saa 5:00 usiku lilipokea taarifa ya ajali ya moto katika mtaa wa Moravian Kata ya Isyesye, ambako askari Polisi walikwenda na kukuta kibanda kikiteketea kwa moto na katika uchunguzi ilibainika mwili wa mtu wa jinsia ya kike ambao wakati huo haukuweza kutambulika na ulipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya.

“Baada ya uchunguzi wa kitabibu na kuhusisha ndugu ilibainika mwili huo ni wa Shairose Mabula aliyeripotiwa kupotea,” alisema.

Alisema wanaendelea na uchunguzi wa kina ukiwamo wa kisayansi ili kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.

Ametoa wito kwa jamii kwa yeyote mwenye taarifa zitakazofanikisha kuwakamata watuhumiwa aziwasilishe, huku akiiasa kutojichukulia sheria mkononi.

Linagroli Rafael, aliyesoma Shule ya Sekondari Panda Hill, jijini Mbeya, pamoja na Shairose amesema hakustahili kufanyiwa unyama huo.

Akiwa msibani nyumbani kwa kina Shairose, amesema alipenda kushirikiana na wenzake.

“Hili ni pigo la kwanza kwangu kupoteza mtu wangu wa karibu tuliyeishi vizuri maisha ya nje na ndani ya darasa, alikuwa mtulivu,” amesema.

Tumpale Frank, amesema Shairose alikuwa mcheshi kwa kila mtu hakuwa mwenye majivuno au kufanya jambo kinyume cha maadili ya jamii.