Unguja. Mgombea ubunge wa Jimbo la Chaani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ayoub Mohamed Mahmoud ameahidi kutekeleza mkakati wa maendeleo wenye nguzo nne kuu endapo atachaguliwa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza leo Ijumaa, Septemba 19, 2025, katika Jimbo la Chaani uliofanyika Bandamaji, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub amesema nguzo hizo ni kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza ufaulu wa wanafunzi, kudumisha mshikamano wa kijamii, pamoja na kuboresha miundombinu ya kiuchumi na huduma za kijamii.
Kuhusu usalama wa chakula, ameeleza kuwa atahakikisha kila mwaka tani 100 za chakula zinahifadhiwa ili kukabiliana na uhaba unaolikabili jimbo hilo.

Mgombea Uwakilishi Chaani, Juma Usonge Hamad akizungumza katika mkutano Mkuu wa Jimbo la hilo. Picha na Zuleikha Fatawi
Kila wadi itapewa kontena maalumu la kuhifadhia chakula hicho ili kiweze kutumika wakati wa dharura au misimu ya upungufu.
“Tunahitaji kuhifadhi tani 100 za chakula kwa mwaka na kila wadi tutaweka kontena. Hii ni hatua ya kuweka akiba kwa dharura na kuondokana na upungufu wa chakula,” amesema.
Katika sekta ya elimu, Ayoub ameahidi kugharamia ada za kambi za wanafunzi ambazo awali zilibebwa na wazazi, ili kuongeza ufaulu.

Pia atahakikisha jimbo hilo linapata skuli ya elimu ya juu na kuweka utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi waliopata ufaulu lakini wazazi wao hawana uwezo wa kugharamia masomo.
Aidha, amesisitiza haja ya mshikamano wa kijamii akisema si busara viongozi kuwagawa wananchi kwa maslahi binafsi. Pia ameahidi kuanzisha saccos yenye vifaa vya kilimo ili wananchi walime kwa tija.
Kwa upande wake, mgombea uwakilishi, Juma Usonge Hamad, amesema lengo la mkutano huo ni kuondoa mgawanyiko uliotokana na kura za maoni na kudumisha mshikamano.
Ameahidi pia kushirikisha viongozi na wajumbe katika kuamua miradi ya maendeleo pamoja na kusimamia upatikanaji wa maji safi na salama. Mwenyekiti wa kampeni, Maryam Muharram, amehimiza mshikamano na umoja baada ya kura za maoni ili chama kishinde kwa kishindo.