Mtindo wa maisha unavyopaisha thamani ya kuku

Dar es Salaam. Katika miji na vijiji vya Tanzania, kuku wameendelea kuwa zaidi ya chakula mezani, ni tegemeo la maisha, chanzo cha ajira na kipato cha uhakika kwa maelfu ya wananchi.

Biashara ya kuku wa nyama imekua kwa kasi, ikichochewa na ongezeko la mahitaji na mabadiliko ya mtindo wa maisha.

Baadhi ya wateja siku hizi hawataki tena kuku mzima, bali huchagua vipande wanavyotaka, hali inayoongeza msukumo wa biashara hiyo.

Lakini safari ya kipato cha mfanyabiashara wa kuku haikomi kwenye mauzo ya nyama pekee. Miguu, utumbo na hata vichwa (vitu ambavyo wengine huona havina maana) navyo vimebeba thamani yake. Kila kipande kina mnunuzi, na kila siku vinaendelea kumwingizia mfanyabiashara fedha kidogo kidogo, na kwa kuzikusanya, si haba kwa kile apatacho.

Rashid Abdul, maarufu Mr Kuku, mkazi wa Ilala anayefanya biashara zake eneo hilo, anasema ana miaka mitano katika biashara ya vipande vya kuku, ambayo hatamani kuiacha kutokana na faida apatayo.

“Kuku ninaouza nachukua Ilala kwa sababu nimezoeana na wauzaji pamoja na wachinjaji, huwa wananifanyia bei rahisi tofauti na wengine,” anasema.

Anasimulia kwamba kwa siku hununua kuku 70, wote huisha. Kipindi cha sikukuu, hununua hadi kuku 100 kutokana na idadi ya wateja kuwa kubwa.

Awali alikuwa akiuza chipsi na kuku wasio na viungo, lakini mahitaji ya wateja yalikuwa tofauti.

“Siku moja alikuja mteja akahitaji kuku, akaomba aweke ndimu, ukwaju na pilipili. Hayo yalipofanyika, ladha ikabadilika, akasema kuku wangu mtamu mno, akaniuliza kwa nini usiuze kwa mtindo huo?” anasema.

Ni kutokana na ushauri huo, alitanua biashara kwa kuanza na kuku 20 aliowachoma na wengine kuwakaanga. Wale wa kuchoma walikuwa na wateja wengi zaidi kuliko wa kukaanga.

Mapokeo hayo ya wateja yalimfanya aongeze idadi ya kuku kutoka 20 hadi 40. Kadri siku zilivyosonga, alizidi kuongeza idadi kwa kuwa oda ziliongezeka kutoka maeneo mbalimbali.

Mr Kuku anasema hununua kuku mmoja kwa Sh6,500 na hulipa Sh300 kwa mchinjaji. Huuza kuku kwa namna tatu— mzima, nusu na robo kulingana na oda ya mteja.

Anabainisha kuwa kuku mzima anauza Sh10,000, nusu Sh5,000, robo ya paja Sh2,000, kidari Sh2,500, shingo Sh500, firigisi ikiwa pamoja na utumbo Sh800, miguu pamoja na kichwa Sh500.

Kwa mpangilio huo, tofauti na mauzo ya kuku mzima, yule anayeuza kwa vipande humwezesha kukusanya Sh10,800.

“Awali sikuwa nikiuza kichwa, utumbo wala miguu, lakini niliona vina faida nikaongeza kwenye biashara. Vitu hivyo vinaisha haraka kuliko watu wanavyofikiria kwa sababu wengine hununua pamoja na kachori,” anasema.

Anasema kwa kuwa hutumia mkaa, hununua gunia kwa gharama ya Sh60,000 hadi Sh70,000. Kuhusu jiko, awali alitengeneza eneo la Gerezani kwa Sh60,000, lakini baadaye alinunua lililotengenezwa kwa pipa kwa Sh150,000.

Mr Kuku anasema wale wa kukaanga hutumia umeme na wakati mwingine gesi pale umeme unapokatika. Hufanya biashara kuanzia saa 10:00 jioni hadi saa 7:00 usiku.

Biashara hiyo imemwezesha kulipa kodi ya eneo la biashara, kupata mahitaji ya nyumbani na ya watoto wake wanasoma shule za Serikali.

Kwa upande wake, Raphael Massawe anayefanya biashara hiyo eneo la baa jijini Dar es Salaam anasema: “Gharama ya kuku hapa ni tofauti na mtaani. Hapa siuzi miguu, vichwa na utumbo, hivyo nawaachia wachinjaji.”

Kwa Massawe, kuku mzima anagharimu Sh15,000, nusu Sh7,500 na robo Sh3,000; haijalishi mteja amechukua paja au kidari, gharama ni moja. Hii pia inatumika kwa kuku aliyechomwa au kukaangwa.

Kwa upande wa supu, gharama ya kuanzia ni Sh4,000; kwa siku akifanya biashara ya kuku 100, wateja wakiwa wa ndani na nje ya baa.

Massawe hutumia mkaa kutoka mkoani, humuuzia kwa kati ya Sh45,000 na Sh50,000.

Mafuta hununuliwa ndoo au dumu la lita 20 kwa Sh80,000, ambalo humtumia kwa siku mbili au tatu.

“Siku hizi watu hawapendi mafuta, hupendelea kuku wa kuchoma,” anasema.

Subira Kinyogoli, mfanyabiashara wa kuku Buguruni, anasema huuza 10 kwa siku kwa vipande, akieleza paja huuza Sh2,000 sawa na kidari kisicho na kipapatio, huku vipapatio vitatu huuza Sh500, fungu la utumbo Sh500, mguu na kichwa kila kimoja Sh100, fungu la kitako cha kuku Sh500, fungu la ngozi Sh300, shingo Sh500 na firigisi Sh700.

“Nikienda sokoni nachanganya kuku na mabaki yake, hununua ndoo ndogo kwa kati ya Sh3,000 na Sh5,000 inategemea biashara ya siku hiyo,” anasema.

Anatumia jiko la kawaida la mkaa alilonunua kwa Sh5,000 na hutumia mafuta lita tatu kwa siku kwa gharama ya Sh4,500. Nishati anayotumia ni kuni ambazo hununua fungu Sh1,000, wakati mwingine hupokelewa kwa Sh500.

Mtaalamu wa uchumi, Sophia Musa, anasema biashara ya kuku kwa vipande ni mfano hai wa namna watu wa kipato cha chini wanavyoweza kujikwamua kimaisha mijini.

Mfumo huo unatoa fursa kwa mfanyabiashara kutumia mtaji mdogo kuingia sokoni na kujipatia kipato cha kila siku kinachotosha kugharimia maisha ya familia.

Hii ni kwa sababu biashara inategemea kanuni rahisi ya mgawanyo wa bidhaa, vipande vidogo huuzwa kwa wateja wengi zaidi.

“Biashara hii ni mfano mzuri wa ubunifu katika sekta isiyo rasmi. Mfanyabiashara hahitaji mtaji mkubwa, kinachohitajika zaidi ni nidhamu, usafi na kuelewa mahitaji ya wateja.

“Kwa kufanya hivyo, mtu anaweza kuondoka nyumbani asubuhi na kurudi jioni akiwa na kipato cha kumwezesha kuendesha maisha ya kila siku,” anasema.

Anasema faida ya biashara ya vipande ni kwamba haina upotevu, kila sehemu ya kuku ina soko lake kuanzia miguu hadi kichwa. Hivyo, kila mfanyabiashara ana hakika kuwa bidhaa zake zote zina mnunuzi.

“Kwa mtazamo wa kiuchumi, hii ni biashara yenye uendelevu kwa sababu inawaunganisha wafanyabiashara wadogo na watumiaji wa kipato cha chini. Inawapa nafasi ya kila mmoja kufaidika, muuzaji kupata kipato na mnunuzi kupata protini kwa gharama anayoweza kuimudu,” anasema.

Anasema endapo biashara hiyo itaungwa mkono kwa mafunzo ya usafi na mbinu bora za uhifadhi, inaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana mijini na kupunguza utegemezi wa ajira za ofisini pekee.