Mgombea wa kiti cha Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiwa na Mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wengine, wameshiriki dua maalum ya kumwombea Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, katika kaburi lililopo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar leo tarehe 19 Septemba 2025.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewanasihi viongozi wa dini, waumini wa Kiislamu na wananchi kwa ujumla kuendelea kuiombea nchi amani na utulivu inapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
Alhaj Dkt. Mwinyi ametoa wito huo leo tarehe 19 Septemba, 2025, alipojumuika na waumini wa Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ijitimai Markaz Kianga, Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo pia iliombwa dua maalum kwa ajili ya kulibariki Taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Katika nasaha zake, Rais Dkt. Mwinyi amesema ni wajibu wa waumini kuendelea kuiombea nchi kabla ya Uchaguzi, wakati wa Uchaguzi, na hata baada ya Uchaguzi ili kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa.
Aidha, amewataka waumini na wananchi kwa ujumla kuwaombea dua wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ili Mwenyezi Mungu awajaalie kutekeleza kwa mafanikio ahadi wanazozitoa katika mikutano ya kampeni.
Halikadhalika, Dkt.Mwinyi ameushukuru uongozi wa Taasisi ya Fissabilillah Markaz Kianga Sharkia kwa hatua yao ya kuiombea nchi pamoja na viongozi, na amewataka kuendeleza jitihada hizo za kuliombea Taifa.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi ametoa mchango wa shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa msikiti huo, ili waumini waweze kutekeleza ibada zao katika mazingira bora zaidi.
