Unguja. Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha amewanadi wagombea wa ubunge na uwakilishi wa Jimbo la Makunduchi, akieleza kuwa ndio viongozi wanaostahili kupewa ridhaa na wananchi kutokana na uwezo wao wa kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili jimbo hilo.
Akiwahutubia wakazi wa Makunduchi, Nahodha amewasihi wapiga kura kutofanya kosa siku ya kupiga kura, bali wawachague wagombea wenye dira na dhamira ya kweli ya kuliletea maendeleo jimbo hilo.
Wagombea waliotajwa ni Wanu Hafidh Ameir anayewania nafasi ya ubunge na Haroun Ali Suleiman anayewania uwakilishi.
Nahodha ameeleza kuwa baadhi ya changamoto zinazohitaji kushughulikiwa haraka ni pamoja na ukosefu wa maji safi na salama, pamoja na tatizo la upungufu wa umeme.
Mbali na hayo, amesisitiza kuwa wagombea hao pia wana jukumu la kuinua kiwango cha elimu katika jimbo hilo huku akiwasifu wagombea hao kwamba wana uwezo wa kufanya hayo yote.
Nahodha ametoa kauli hiyo leo, Septemba 19, 2025, wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za uchaguzi kwa Jimbo la Makunduchi, uliofanyika katika Uwanja wa Muyuni, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amewashauri wagombea hao wafanye kila lonalowezekana kunyanyua kiwango cha elimu, maana kuna dalili za kuporomoka kiwango katika jimbo hilo.
Nahodha amesema kazi ya uongozi si ya majaribio kwa hiyo chama hicho ndio kina wagombea waliopikwa na uwezo wa kuleta mabadiliko kwenye maeneo tofauti.
“Hatuwezi kuifanya nchi yetu kuwa kichwa cha mwenda wazimu, tunao wagombea wazuri, tusifanye makosa
“Tunao wajibu kuchagua watu wenye kuleta maendeleo, au tusichague watu kwa majaribio, lakini njia sahihi ni kuwachagua wagombea wa CCM,” amesema.
Nahoda amesema amekuwa kwenye siasa zaidi ya miaka 25 na hakuna chama makini kama kilivyo CCM.
Naye mgombea ubunge, Wanu amesema yaliyotajwa hakuna shaka yatatekelezwa yapo mikononi salama.
“Changamoto za maji na umeme tumesema kwa muda mfupi zitaenda kutatuliwa kwa haraka, najua matatizo yaliyopo katika jimbo hili na hili la elimu sio tatizo tena, Mkoa wa Kusini Unguja unaingia katika shule 10 bora.
“Changamoto zilizotajwa hapa wananchi wasiwe na wasiwasi zinakwenda kupata suluhu, kwani wanasema mzigo mzito mpe mwanamke Mzanzibari,” amesema na kuongeza;
“Nimekuwa na uzoefu wa uongozi kuanzia Umoja wa Vijana mwaka 2008 na mwaka 2010, nikaingia barazani na nimeacha alama kubwa, kwa hiyo mimi ni mtoto wa hapa nyumbani na nimeyaishi maisha, najua matitizo yote,” amesema.
Ametumia fursa hiyo kuwaombea kura viongozi wengine wa chama hicho ngazi ya urais wakiwamo mgombea urais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na mgombea urais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Kwa upande wake mgombea uwakilishi wa Makunduchi, Haroun Ali Suleiman amewaondoa shaka ya kukosa maji kwani suala hilo lipo kwenye mipango ya Serikali.
“Nia tunayo, uwezo tunao wa kukutumikieni bila wasiwasi,” amesema.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani, Mohamed Mchengerwa amesema, “nataka niwathibitishie hamjakosea, changamoto mlizonazo Wanu atazimaliza na mtapiga hatua na ataleta maendeleo.”
Amesema hakuna chama chenye uwezo wa kuleta maendeleo kama CCM na hiyo imejidhihirisha katika uwatala wa Rais Hussein Mwinyi na Samia Suluhu Hassan katika vipindi vya utawala wao.
“Ninawaomba siku ya tarehe 29 twendeni tukawachague viongozi wetu hawa kwa mara nyingine,” amesema