Simchimba, Raizin kuna kitu Mtibwa Sugar

NYOTA wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh amesema kucheza timu moja na mshambuliaji mwenzake, Andrew Simchimba ni jambo nzuri litakaloisaidia kikosi hicho kufanya vizuri zaidi kwa msimu wa 2025-2026 kutokana na kile walichokifanya msimu ulipita.

Kauli ya Raizin inajiri baada ya Simchimba aliyejiunga na Singida Black Stars katika dirisha kubwa la usajili akitokea Geita Gold kutolewa kwa mkopo kwenda Mtibwa Sugar, iliyorejea tena Ligi Kuu baada ya kushuka daraja msimu wa 2023-2024.

Akizungumza na Mwanaspoti, Raizin alisema kucheza na Simchimba ni jambo litakaloongeza ufanisi wa safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho msimu huu, kutokana na viwango vizuri walivyovionyesha msimu uliopita wakicheza Ligi ya Championship.

“Ni mshambuliaji tunayefahamiana sana kwa sababu sio mara ya kwanza pia sisi kucheza timu moja, mashabiki zetu wanapaswa kutambua tulicheza pamoja msimu wa 2017-2018, tukiwa Coastal Union, hivyo ni mchezaji ninayejivunia,” alisema Raizin.

Simchimba alikuwa mfungaji bora wa Championship kwa msimu wa 2024-2025, akiichezea Geita Gold baada ya kufunga mabao 18, sawa na Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar na Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ aliyekuwa TMA Stars, ingawa kwa sasa amehamia Namungo.

Kama utakuwa umesahau pia, Simchimba ni miongoni wa nyota waliowahi kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), msimu wa 2022-2023, alipofunga mabao yake saba, akiwa na kikosi cha Ihefu kwa sasa Singida Black Stars.

Nyota huyo ameiwezesha pia Geita Gold kumaliza ya nne na pointi 56 na kucheza mechi za ‘Play-off’ ili kupanda Ligi Kuu Bara ambapo ilikwama, baada ya kuchapwa na Stand United iliyomaliza msimu ya tatu na pointi 61, kwa jumla ya mabao 4-2.