TBS KUTUMIA BIL. 36 KUJENGA MAABARA ZA KISASA DODOMA, MWANZA

:::::::::

Serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetenga kiasi cha Sh. bilioni 36.8 kwa ajili ya ujenzi wa maabara za kisasa katika mikoa ya Dodoma na Mwanza, ikiwa ni jitihada za kusogeza huduma karibu na wananchi na kupunguza gharama za upimaji wa sampuli.

Akizungumza jana jijini Dodoma katika kikao kazi kilichowakutanisha wahariri wa vyombo vya habari, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, alisema maabara hizo zitakuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya utoaji wa huduma za viwango nchini.

Alisema kuwa maabara zitakazojengwa Dodoma zitatumika kuhudumia mikoa ya Kanda ya Kati ambayo ni Dodoma, Singida na Tabora, wakati zile za Mwanza zitahudumia mikoa sita ikiwemo Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.

“Ujenzi wa maabara hizi utasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi, jambo litakaloboresha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika upimaji wa sampuli,” alisema Dkt. Katunzi.

Kwa mujibu wa Dkt. Katunzi, TBS tayari ina jumla ya maabara 12 zilizopata ithibati ya umahiri na vyeti vya kimataifa, hatua inayothibitisha kuwa majibu yanayotolewa na maabara hizo yanakubalika kimataifa.

Akitaja uwekezaji katika vifaa, Dkt. Katunzi alisema kuwa serikali imetumia zaidi ya Sh. bilioni 12.9 kununua mashine za kisasa (state-of-the-art equipment) kwa ajili ya maabara hizo.

Baadhi ya mashine hizo ni Hydrostatic Pressure Test Machine, inayotumika kupima mabomba ya maji kuanzia kipenyo cha inchi 0.5 (mm 12) hadi inchi 32 (mm 800), na yenye uwezo wa kupima hadi sampuli 120 kwa wakati mmoja. Mashine hiyo inapatikana katika nchi tano pekee barani Afrika, zikiwemo Tanzania.

Mashine nyingine ni Automatic Conductor Resistance Tester, inayopima waya za umeme wa aina zote hadi kipenyo cha milimita 40 au milimita za mraba 1,200, pamoja na Solar Simulator, inayopima ubora wa paneli za sola bila kutegemea mwanga wa jua. Mashine hii, kwa sasa, inapatikana Tanzania pekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Aidha, TBS imetenga kiasi cha Sh. milioni 350 kila mwaka kwa ajili ya kusaidia wajasiriamali wadogo na wa kati kufanikisha uthibitisho wa ubora wa bidhaa zao.

“Huduma hii hutolewa kwa kuzingatia mahitaji ya kila halmashauri. Tutaendelea kushirikiana na watendaji wa halmashauri ili kuwatambua wajasiriamali wanaohitaji huduma hizi lakini hawana uwezo wa kifedha,” alifafanua Dkt. Katunzi.

Aliongeza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha bidhaa za wajasiriamali wa ndani zinatimiza viwango bora na kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Katunzi aliwataka wazalishaji na waingizaji wa bidhaa nchini kuhakikisha wanafuata taratibu zilizowekwa na Serikali kupitia TBS, ili kuhakikisha bidhaa zinazowafikia wananchi ni salama na zenye ubora.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena alilishauri TBS kuendelea kushirikiana kwa karibu na waandishi wa habari kwa kuwaelimisha kuhusu masuala ya viwango.

“Ushirikiano wa karibu kati ya TBS na vyombo vya habari utasaidia kuelimisha umma na kuongeza uelewa wa masuala ya viwango,” alisema Meena.