TEC yatoa taarifa misa ya kumuaga Askofu Mkuu Rugambwa

Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limetoa taarifa ya mazishi ya Askofu Mkuu, Novatus Rugambwa, aliyekuwa Balozi wa Papa nchini New Zealand.

Askofu Mkuu Rugambwa alifariki dunia Septemba 16, 2025 akiwa Roma, nchini Italia.

Taarifa hiyo iliyotolewa leo Septemba 19, 2025 imeeleza Sekretarieti ya TEC inawafahamisha makardinali, maaskofu wakuu, maaskofu, mapadri, watawa na waamini wote kuwa misa ya kumuaga Askofu Mkuu Rugambwa itafanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam, Jumamosi Septemba 27, saa 3:00 asubuhi.

TEC, katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Padri Clement Kihiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa baraza hilo, limesema misa ya mazishi ifanyike Kanisa Kuu Jimboni Bukoba, Jumatatu Septemba 29, saa 3:30 asubuhi.

Askofu Mkuu Rugambwa alizaliwa Oktoba 8, 1957, katika Jimbo Katoliki la Bukoba, nchini Tanzania. Baada ya masomo na majiundo ya kikasisi, akapewa daraja takatifu ya upadri mikononi mwa hayati Askofu Nestorius Timanywa Julai 6, 1986.

Juni 10, 2025, akiwa mgonjwa, Askofu Mkuu Rugambwa alishiriki mkutano wakati Papa Leo XIV alipokutana na mabalozi wote wa Vatican wanaomwakilisha maeneo yote duniani. Alikuwa akitumia kitimwendo.