:::::::::
Mamlaka ya Uwekezaji pamoja na Maeneo Maalum ya Uwekezaji (TISEZA) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Benki ya Tanzania Commercial Bank (TCB) kwa lengo la kutoa huduma bora na za haraka za kifedha kwa wawekezaji wanaotembelea mamlaka hiyo.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini ya makubaliano hayo iliyofanyika makao makuu ya TISEZA jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Bw. Gilead Teri, alisema makubaliano hayo yanalenga kusogeza huduma bora za kifedha karibu zaidi na wawekezaji, ikiwemo kuongeza wigo wa huduma kwa wawekezaji wa ndani na wa nje.
“Makubaliano haya yatakuwa katika nyanja mbalimbali, ambapo mwekezaji atafahamu kuwa huduma bora za kifedha zipo kupitia mshirika wetu wa kibenki, Benki ya TCB,” alisema Bw. Teri.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Bw. Adam Mihayo, alisema benki hiyo imekuwa ikitoa huduma kwa wateja wa kawaida kwa muda mrefu, lakini sasa imedhamiria kuwasaidia wawekezaji kwa kutoa suluhisho la haraka na linalowafaa katika huduma za kifedha.
Bw. Mihayo aliahidi kuwa TISEZA imechagua mshirika sahihi katika benki ya TCB, na ushirikiano huu utaongeza ufanisi katika huduma kwa wawekezaji, hivyo kuchochea ukuaji wa uwekezaji nchini.