Tabora. Mkoa wa Tabora unatarajiwa kunufaika na ujenzi wa viwanda vya mbolea na cha kuchakata tumbaku ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ya chakula na biashara sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla. Viwanda hivyo vinatarajiwa kujengwa katika kipindi kifupi kijacho, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Ujenzi wa viwanda hivyo unatarajiwa kuongeza ajira kwa wananchi, kuinua kipato cha wakulima wa Tabora, na kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao husika, hususan zao la tumbaku ambalo ni moja ya mazao makuu ya biashara mkoani humo.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Septemba 19, 2025, na mgombea ubunge wa Jimbo la Nzega Mjini ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni za kunadi sera za Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Tabora inalimwa tumbaku nyingi, ni lazima tuwe na kiwanda na ujenzi hivi karibuni utaanza. Kiwanda cha mbolea pia ujenzi unaanza hivi karibuni na eneo tayari limepatikana pale Kata ya Ifucha, hapahapa manispaa. Serikali imefanya kazi kubwa, hivyo tukichague Chama cha Mapinduzi kuanzia Rais mpaka madiwani ili kazi nzuri ziendelee,” alisema Bashe.

Wananchi wa Manispaa ya Tabora wakimsikiliza mgombea ubunge wa Jimbo la Nzega Mjini ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Hussein Bashe, katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika leo Ijumaa Septemba 19, 2025. Picha na Hawa Kimwaga.
Ameeleza kuwa Tabora ni miongoni mwa mikoa iliyokuwa na changamoto nyingi za mahitaji muhimu kama maji ya kutosha, miundombinu bora ya barabara na vitu vinavyoweza kuchochea uchumi kukua kwa haraka.
Aidha, mgombea wa ubunge kwa tiketi ya CCM Jimbo la Tabora Mjini, Hawa Mwaifunga, amesema akichaguliwa kuwa mbunge wa Tabora Mjini atahakikisha mikopo ya asilimia kumi inatolewa kwa usawa kwa wote wenye vigezo ili kila mmoja anufaike.
“Lengo la Serikali ni kuinua wananchi wake kiuchumi, hivyo fedha hizo zinakuja mahsusi kwa ajili ya hilo. Nitazisimamia ili kila mmoja aweze kunufaika nazo, tufikie mahali kila mmoja awe vizuri kiuchumi na aifurahie serikali yake,” alisema.
Mwaifunga aliongeza kuwa Kata ya Gongoni ipo katikati ya Tabora Mjini, hivyo ni lazima barabara zake ziwe za viwango vya juu. Alisisitiza kuwa licha ya kuwepo kwa barabara nyingi za lami, bado kuna barabara zisizokuwa na lami ambazo lazima zijengwe kwa kiwango bora ili kuendana na uzuri wa mji.
Kwa upande wake, mgombea wa udiwani kupitia CCM Kata ya Gongoni, Kessy Abdurahmani, amewaomba wananchi wamchague mgombea wa urais kupitia chama hicho, Samia Suluhu Hassan, mgombea ubunge Tabora Mjini Hawa Mwaifunga, na yeye kama diwani wa kata hiyo.
Amesema wakipata ridhaa ya wananchi wataisimamia vyema Ilani ya chama hicho ambayo inatekelezeka na imegusa mahitaji ya wananchi, ikiwemo maboresho ya sekta za afya, elimu, miundombinu na huduma zingine za kijamii.