Watawa waliofariki ajalini wazikwa Dar

Dar es Salaam. Watawa wanne waliofariki dunia katika ajali ya gari mkoani Mwanza, wamezikwa  leo Septemba 19 jijini Dar es Salaam na jamii imetakiwa kuwakumbuka kwa kuishi vema kwa kuacha alama.

Waliofariki dunia katika ajali hiyo iliyotokea Septemba 15, 2025 mkoani Mwanza baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori, ni Lilian Kapongo, aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Watawa Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Duniani, Nerina De Simone, katibu wa shirika hilo duniani; Damaris Matheka, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bukumbi na Stellamaris Muthini aliyehudumu katika utume wa Kimisionari Kenya.

Katika ajali hiyo, dereva wa watawa hao, Boniphace Msonola, pia alifariki dunia na mwili wake ulizikwa Septemba 18 Nyegezi, jijini Mwanza.

Majeneza yenye miili ya masista wanne wa waliofariki ajalini Mwanza ikiwa katika Kanisa la Mwenyeheri IsdorI Bakanja Boko, Jimbo Katoliki Bagamoyo kwa ajili ya misa ya kuwaombea kabla ya maziko.

Maziko ya watawa hao yamefanyika leo Ijumaa Septemba 19, 2025 katika Kituo cha Kiroho cha Mtakatifu Teresa wa Avila, Boko, yakitanguliwa na misa ya kuwaombea iliyofanyika katika Parokia ya Mwenyeheri Isidori Bakanja, iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi.

Katika mahubiri, Askofu wa Jimbo la Bagamoyo, Stephano Musomba amesema wanawazika watawa hao kwa kusema buriani, lakini waliyoyafanya yatabaki mioyoni kwa kuwa wameacha alama isiyofutika.

“Kama tulivyosikia katika wasifu wa dada zetu wanne hapa, tumeyaona yote waliyoyatenda, tumeziona kazi zao njema walizozifanya katika shirika na katika jamii yetu. Kwa sababu hiyo, wapo vichwani mwetu na wapo katika akili yetu, tunawakumbuka,” amesema na kuongeza:

“Kwa hiyo kwenye kufa kunaweza kuwa na sehemu mbili zote, kufa Mungu amewapokea awe nao milele, lakini kwetu sisi hawatapotea katika kumbukumbu zetu kwa sababu tunayaona matendo yao, tunaona alama zilizowekwa na wao kwetu.”

Amesema: “Kwa sababu hiyo, kifo cha masista hao ni kama sadaka ya kuteketeza inayompendeza Mungu, licha ya kwamba hawaonekani, ukweli ni kwamba wamepoteza maisha yao ya duniani, lakini wapo mbinguni.”

Majeneza yenye miili ya masista wanne wa waliofariki ajalini Mwanza ikiingizwa katika Kanisa la Mwenyeheri IsdorI Bakanja Boko, Jimbo Katoliki Bagamoyo kwa ajili ya misa ya kuwaombea kabla ya maziko.

Makamu Mkuu wa shirika hilo la watawa nchini Tanzania, Sista Vestina Tibenda, amesema wanamshukuru Mungu kwa wito wa utawa aliowapatia na kutoa maisha yao yote kwa Mungu kwa moyo wa imani na kijasiri.

“Tunaposhukuru leo kwa kazi za masista hawa, tunashukuru na kukiri kwamba kazi ya Mungu haina makosa. Tunashukuru kwa zawadi ya maisha ya dada zetu hawa ambao ni maua ya kwanza yaliyochumwa na Mungu katika bustani ya Karmeli barani Afrika, tukiamini miito itaongezeka katika shirika na kanisa kwa maombezi yao,” amesema.

Amewashukuru wazazi na walezi wa masista hao waliowalea katika imani, sala zao na ridhaa ya kuwaruhusu wawe zawadi kwa familia ya kitawa na kwa kanisa.

Vilevile, amelishukuru kanisa kwa ushiriki wake katika kipindi kigumu kwao, akiwamo Askofu wa Jimbo Katoliki la Mwanza pamoja na mapadri waliokuwa wa kwanza kuwakimbilia ajali ilipotokea na kuratibu mipango yote ya kuhifadhi miili na kuadhimisha misa ya kuwaombea na kuwaaga.

Mbali ya viongozi wa dini, waamini na waombolezaji wengine, maziko hayo yamehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambalike.

Chalamila akitoa salamu, amewasilisha Sh20 milioni kati ya fedha hizo, Sh10 milioni amesema ni kwa ajili ya rambirambi na Sh10 milioni ni kwa ajili ya kuendeleza ukarabati wa kanisa.