Yanga mwendo mdundo, yaizima Wiliete kwao

‘NO Aucho No problem!’ Ndivyo mashabiki wa Yanga kwa sasa wanatamba mtandaoni, baada ya kiungo mkabaji, Aziz Andabwile kugeuka lulu kikosini na kuendelea kuwapa raha pale jana alipofunga bao tamu wakati timu hiyo ikiizamisha Wiliete Benguela ya Angola kwa mabao 3-0.

Katika mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa kwenye Uwanja Novemba 11, Luanda Angola mabao mengine yaliwekwa kimiani katika kipindi cha pili na mtokea benchini Edmund John na Prince Dube na kuiweka Yanga pazuri kwa mechi ya marudiano.

Andabwile ambaye hakuwa na nafasi katika kikosi cha kwanza kwa msimu uliopita, amegeuka lulu kwa sasa chini ya kocha Romain Folz akimtumia katika eneo la kiungo na hajamuangusha kwani katika mechi ya iliyopita ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba kiungo huyo aliupiga mwingi na kuwafanya mashabiki wa Yanga kumsahau Khalid Aucho aliyekuwa injini ya timu hiyo kwa misimu minne.

Aucho kwa sasa yupo Singida Black Stars, lakini Andabwile anawaka Jangwani na kuwakalisha benchini Mousa Balla Conte aliyesajiliwa hivi karibuni kutoka CS Sfaxien ya Tunisia na jana alifunga bao la kwanza katika kipindi cha kwanza kwa shuti kali dhidi ya wenyeji walio chini ya kocha Bruno Ferry aliyewahi kuinoa Azam FC.

Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, Yanga ilitengeneza nafasi sita za wazi ambazo hata hivyo ilishindwa kuzitumia kabla ya Andabwile kufunga la kuongoza, zikiwamo nafasi tatu ambazo alipoteza Prince Dube.

Dube alipoteza nafasi hizo, ndani ya dakika 20 za kipindi cha kwanza kufuatia Yanga kufanya mashambulizi mfululizo huku Mamadou Doumbia na Pacome Zouzoua wakiwa mwiba kwa Wiliete ambao muda mrefu walikuwa wakicheza katika eneo lao.

Kila Wiliete ilipokuwa ikivuka eneo lao, Yanga ikiwa na Andambwile kwenye eneo la kiungo pamoja na Duke Abuya walifanya kazi nzuri ya kunyang’anya mpira na kuifanya timu hiyo kuwa ngumu kupitika katikati.

Yanga ilipata bao lake la kwanza katika dakika ya 32 kufuatia juhudi binafsi za kiungo, Andabwile ambaye alinyang’anya mpira na kuachia mkwaju mkali wa nje ya boksi ambao ulimshinda kipa wa Wiliete, Agostinho Calunga.

Katika dakika ya 59, kocha wa Yanga, Romain Folz ilifanya mabadiliko mawili kwa mpigo, aliwatoa Clement Mzize na Mamadou Doumbia na kuingia, Maxi Nzengeli na Edmund John. Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na taji kwani ndani ya dakika 20 za cha pili, Edmund aliyekuwa akishambulia kutokea pembeni, alipoteza nafasi moja akimbabatiza kipa, Agostinho lakini pia alikuwa na shuti moja ambalo lililenga lango kabla ya kufunga bao lake la kwanza akiwa na Yanga.

Nyota huyo mpya aliyesajiliwa kutoka Singida Black Stars alipachika bao hilo katika dakika ya 72 kufuatia asisti ya Maxi.

Mabadiliko mengine ya Yanga ambayo yalifanywa katika kipindi hicho cha pili ilikuwa ni pamoja na kutolewa kwa Pacome, Aziz Andabwile na Chadrack Issaka Boka huku wakiingia Balla Moussa Conte, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Celestin Ecua.

Kocha Romain Folz aliamua kufanya mabadiliko ya wachezaji watatu katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo ambacho kiliivaa Wiliete huko Angola, tofauti na kile ambacho kilianza katika Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, Septemba 16.

Yanga ambayo ilitupa karata yake ya kwanza katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikisaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi, ilikuwa mechi ya kwanza kwa Folz kimataifa akiwa na kikosi hicho ambacho siku chache zilizopita alikiongoza kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba bao 1-0.

Mabadiliko hayo yaligusa maeneo mawili tofauti, moja ni ukuta ambapo alitoa nafasi kwa nahodha mkuu, Bakari Mwamnyeto kuongoza jahazi akichukua nafasi ya Dickson Job akicheza sambamba na Ibrahim Hamad ‘Bacca’.

Eneo jingine ni ushambuliaji ambapo, aliamua kuanza na Clement Mzize badala ya Maxi Nzengeli huku pia akitoa nafasi kwa Mamadou Doumbia badala ya Mudathir Yahya.

Yanga inajiandaa kurejea nchini ili kuwahi mechi tya Ligi Kuu dhidi ya Pamba Jiji itakayopigwa Septemba 24 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kisha kurudiana na Wiliete siku chache baadae na ikifuzu hapo itakumbana na mshindi wa mechi kati ya Elgeco Plus ya Madagascar na Silver Strikers ya Malawi katika raundi ya pili kusaka tiketi ya makundi ya michuano hiyo.

Kwa misimu miwili iliyopita ya Ligi ya Mabingwa, Yanga ilifuzu makundi ikiwa chini ya kocha Miguel Gamondi aliyepo Singida BS kwa sasa.

WILIETE: Agostinho, Tobias, Karanga, Mule, Yano, Danilson, Giovani, Edy Maieco, Cairo, Junior na Quare

YANGA: Diarra, Mwenda, Boka/Tshabalala, Mwamnyeto, Bacca, Andabwile/Conte, Mzize/Edmund, Abuya, Dube, Doumbia/Maxi na Pacome/Ecua