KOCHA wa Geita Gold, Zubery Katwila, amesema kipaumbele chake cha kwanza ni kuhakikisha anaipambania timu hiyo kurejea tena Ligi Kuu, baada ya kushindwa kutimiza malengo hayo msimu uliopita, licha ya kucheza pia mechi za mtoano ‘Play-Off’.
Katwila aliyetamba na timu mbalimbali zikiwemo, Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na Mtibwa Sugar, amejiunga na Geita Gold kwa mkataba wa mwaka mmoja, baada ya kuachana na Bigman, aliyojiunga nayo msimu uliopita wa Championship.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katwila alisema licha ya changamoto na vipaumbele vya kuhakikisha anakirejesha tena kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara, ila hana wasiwasi kutokana na aina ya usajili wa wachezaji wapya waliojiunga na timu hiyo.
“Kitu kikubwa nilichowaomba viongozi wakifanye kabla sijaja ni kuhakikisha wachezaji wote bora waliofanya vizuri msimu uliopita wanabaki na kuongezea wengine, nashukuru suala hilo lilizingatiwa ndio maana nikajiunga nao,” alisema Katwila.
Kwa msimu wa 2024-2025, Katwila aliiwezesha Bigman kumaliza ikiwa nafasi ya nane katika Ligi ya Championship na pointi 47, baada ya kushinda mechi 12, sare 11 na kupoteza saba, ikifunga mabao 29 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 21.
Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu wa 2024-2025 katika Ligi ya Championship ilimaliza ikiwa nafasi ya nne na pointi 56 chini ya Kocha Mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kupanda Ligi Kuu Bara, baada ya kufeli mechi za ‘Play-off’.
Timu hiyo ilicheza ‘Play-off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2 kisha kuchapwa ugenini 2-0.
Miongoni mwa nyota wapya waliojiunga na timu hiyo ni aliyekuwa beki wa Yanga, Ali Ali aliyeungana tena na Kocha, Katwila baada ya kufanya kazi wote Bigman, Maulid Shaban (Coastal Union), Said Mbatty na Mtenje Albano waliotokea Fountain Gate.