Arusha. Licha ya jaribio la kunywa sumu ya kuulia wadudu kwa lengo la kujiua baada ya kumuua mkewe, Rehema Daniel, kwa kumkata kwa panga, Peter Deus hakuweza kuukwepa mkono wa sheria.
Baada ya sumu hiyo kuanza kumletea maumivu makali tumboni, alipiga simu polisi kuomba msaada.
Tukio hilo lilitokea Septemba 24, 2023, katika Kijiji cha Njiapanda, eneo la Ungayang’ombe, wilayani Igunga, mkoani Tabora. Inadaiwa kuwa Peter alimuua mkewe kutokana na mgogoro wa kifamilia uliohusisha wivu wa kimapenzi.
Kwa mujibu wa maelezo ya onyo aliyotoa polisi, Peter alikiri kumuua mkewe kwa kumkata kwa panga kichwani, mikononi na miguuni, kisha kumuacha akiwa anatokwa na damu nyingi.
Kwenye maelezo ya onyo, alidai sababu za kufanya hivyo ni hisia zake kwamba mkewe alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na baba mkwe wake (baba mzazi wa Peter).
Baada ya tukio hilo, Peter aliondoka eneo hilo akiwa na panga lenye damu na kuelekea nyumbani kwake, akiwa njiani aliamua kujiua kwa kunywa sumu ya kuulia wadudu aliyokuwa ameibeba, lakini baada ya kuinywa na kupata maumivu ya tumbo ambayo alishindwa kuyavumilia, alipiga simu kituo cha polisi cha Nkinga kuomba msaada.
Polisi kutoka kituo hicho walimkamata akiwa na panga hilo, na kumuwahisha Hospitali ya Rufaa ya Nkinga kwa matibabu, baadaye alifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la mauaji.
Kesi hiyo ya jinai ilikuwa ikisikilizwa Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Tabora mbele ya Jaji Frank Mirindo, aliyetoa hukumu hiyo Septemba 18, 2025 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Mirindo alisema Mahakama imemkuta Peter na hatia ya mauaji ya mkewe na inamhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Katika kesi hiyo, shahidi wa tatu, Dk Modestus Masinde, aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, alithibitisha kuwa kifo cha Rehema kilitokana na kuvuja damu nyingi kutokana na majeraha ya kukatwa na kitu chenye ncha kali.
Ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa Septemba 22, 2023, Rehema (marehemu kwa sasa) alienda kuwaona wazazi wake na kueleza kuwa hatarudi kwa mumewe kwa sababu amekuwa akimpiga.
Peter alieleza Mahakama kuwa tangu 2019 walikuwa wanandoa na mkewe, ila mwaka 2023 aligundua mke wake ana mahusiano ya kimapenzi na baba yake (Peter).
Peter, aliyeieleza Mahakama kuwa hajui kusoma wala kuandika, alidai ugunduzi huo ulitokana na yeye kuchukua simu ya mkononi ya mkewe na kumpa rafiki yake, Mayunga Maguru, ambaye alisomea ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) uliotoka kwa baba yake mtuhumiwa, akimshukuru Rehema kwa kufanya naye mapenzi.
Baada ya hilo kugundulika Septemba 2023, alidai Rehema alitoweka nyumbani na baada ya juhudi za kumtafuta kuendelea, alijulishwa Rehema yuko Singida na baadaye alirejea nyumbani kwao.
Alidai alikwenda kwao na kumsihi arudi nyumbani, lakini Rehema alishikilia kuwa mazungumzo hayawezi kufanyika bila baba wa mshtakiwa kuwepo.
Alidai siku iliyofuata alimfuata baba yake, aliyekuwa akiishi Kitongoji cha Monde, Kijiji cha Nkinga, kumuomba aende naye nyumbani kwa akina Rehema kwa ajili ya kikao, ila alikataa.
Peter alieleza Mahakama siku ya Ijumaa alikwenda kwa akina Rehema na kumweleza kuwa baba yake amekataa kwenda kwenye kikao, ila Rehema hakujibu.
Siku ya tukio, ilidaiwa wakiwa katika kikao, Rehema alidai kuwa baba yake Peter ndiye aliyempa pesa ya kwenda Singida bila kuweka wazi sababu ya kupewa fedha hizo, na alipoulizwa kama kuna jambo lolote baya alilofanyiwa na Peter, alinyamaza.
Kupitia maelezo yake ya onyo, Peter alikiri kumuua mkewe baada ya kukasirishwa na maumivu ya mapenzi na alichukua panga lililokuwa limefungwa kwenye baiskeli.
Akizungumzia kuhusu kurushiana maneno kwa hasira kati ya Rehema na yeye kwenye kikao siku ya tukio, Peter alidai kukasirika baada ya mkewe kumjibu kwa maneno: “Umeolewa na wangapi, mbona unaning’ang’ania sana?”
Sehemu nyingine ya onyo la Peter alinukuliwa akieleza kuwa mkewe alitoroka nyumbani kwa wiki mbili na kwenda Singida kwa dada yake, alikaa kabla ya kurejea kwa wazazi wake.
Alieleza baada ya baba yake kukataa kumsindikiza, alimuomba shemeji yake Jumanne amsindikize. Alivaa koti jeusi, suruali nyeusi na viatu vyeusi, na panga aliliweka ndani ya koti ambapo alilibeba kama silaha endapo mkewe akikataa kurudi, amkate nalo.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, jaji huyo amesema inaonesha mshtakiwa alijizatiti kwa kubeba panga na kwenda nalo ukweni, hivyo alikusudia kuua.
Amesema kupitia ushahidi wa mashtaka na maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo, ambaye alikiri kumuua mkewe, upande wa mashtaka umethibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka.
Jaji Mirindo amesema Mahakama hiyo imemtia Peter hatiani kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.