Bado Watatu – 34 | Mwanaspoti

BABA akasema: “Wewe ukisema unamtuhumu mke wako, sisi tutatoa sababu za kukutuhumu wewe. Sasa ukweli wataujua polisi. Nyote mtapata shida, kwa sababu kama ni kesi itawahusu nyote — hasa wewe, Sufiani!”
Sufiani akanyamza kimya.
Hapo simu yangu ikaita. Nilipotazama skrini ya simu, nikaona jina la Raisa. Nikajisogeza pembeni kidogo kisha nikaipokea.
“Hello… Raisa, vipi?”
“Nimepata taarifa ya kunishitua, shoga…” Raisa akaniambia kwenye simu.
“Taarifa gani?”
“Mjane wa marehemu Shefa amenipigia simu sasa hivi. Ameniambia kuwa unakuja kukamatwa. Polisi wamegundua kuwa wewe ndiye uliyemuua Shefa.”
“Hao polisi wamejuaje?” nikamuuliza huku moyo ukianza kunienda mbio.
“Simu iliyokutwa mfukoni mwa marehemu ndiyo iliyofichua kila kitu. Namba ya mwisho ambayo Shefa aliwasiliana nayo ni namba yako. Polisi walikwenda katika kampuni ya simu kufanya utafiti ili kumjua mmiliki wake. Kule walionyeshwa picha yako na kutajwa jina lako, na pia kampuni ya simu iliwapa polisi kipande kilichorekodiwa cha mazungumzo yenu na Shefa.”
“Unasema kweli, shoga. Mazungumzo yetu pia wamepewa polisi?”
“Waliyaomba kama ushahidi. Mimi nimerushiwa na mjane wa Shefa. Sauti ya Shefa inasikika ikikwambia kuwa anakuja nyumbani kwako. Wewe ukajibu kwamba usije muda huu, njoo saa sita.”
Hayo mazungumzo niliyazungumza kweli na Shefa. Sasa nikajua ninakuja kukamatwa kweli.
“Sasa shoga, nakuja huko tuzungumze vizuri,” nikamwambia.
“Sawa, nakusubiri.”
Raisa akakata simu. Pale nilipata wazo moja tu: nitoroke pale nyumbani ili nisije nikakamatwa. Niliingia chumbani, nikachukua nguo zangu chache pamoja na vitu vyangu muhimu, nikavitia kwenye begi dogo kisha nilichukua pesa zangu za akiba na kuzitia kwenye pochi yangu. Nikatoka.
“Unakwenda wapi?” Baba yangu akaniuliza.
“Nimeambiwa polisi wanakuja kunikamata, nakimbia,” nikamjibu huku nikitembea kwa haraka kuelekea kwenye mlango.
“Nani aliyekwambia?”
“Raisa…”
Nilifika mlangoni, nikaufungua na kutoka.
“Hebu rudi kwanza,” niliisikia sauti ya baba akiniambia, lakini nilitoka, nikafunga mlango na kutembea haraka kuelekea mtaa wa pili.
Katika mtaa huo kulikuwa na kituo cha bodaboda. Nikakodi mojawapo na kumwambia aliyekuwa akiendesha anipeleke Kwaminchi. Nilikusudia kwenda kwa Raisa.
Baada ya robo saa, bodaboda ikanishusha Kwaminchi, mbele ya nyumba aliyokuwa akiishi Raisa.
Nilibisha mlango. Raisa akanifungulia.
“Karibu,” akaniambia huku akinitazama usoni.
Niliingia ndani na kufika kwenye sebule yake.
Raisa alifunga mlango na kuniambia, “Karibu ukae.”
Nilikaa kwenye sofa nikaliweka begi langu kando yangu.
“Shoga, hebu nieleze vizuri yale maneno,” nikamwambia.
“Naona, shoga, nimekushitua sana. Lakini usinilaumu mimi. Jilaumu mwenyewe,” Raisa akaniambia.
“Kwanza naomba unieleze tena yale maneno, halafu nitakueleza ukweli wangu.”
Raisa akanieleza tena. Sasa akanieleza kwa utulivu zaidi. Maneno yakaingia kichwani mwangu.
Aliniambia kuwa ile simu ya Shefa ambayo ilikutwa mfukoni mwake wakati mwili wake ulipoonekana kule makaburini, ilibaki mikononi mwa polisi kwa ajili ya uchunguzi.
Polisi walitafuta namba ambazo marehemu aliwasiliana nazo usiku wa siku ile aliyotoweka kabla ya mwili wake kuokotwa.
Wakakuta aliwasiliana na namba yangu saa tatu usiku.
Baada ya kupata namba yangu, polisi walikwenda katika kampuni ya simu kuulizia ile namba ilikuwa ya nani na pia kujua usajili wake.
Huko ndiko walikopata jina langu, picha yangu na anuani yangu. Kwa msaada wa kampuni ya simu, iliwapa polisi kipande cha mazungumzo ambayo nilizungumza na Shefa usiku ule.
Raisa aliniambia kipande hicho alirushiwa naye kwenye mtandao wa WhatsApp na akanifungulia kutoka kwenye simu yake; nikayasikia mazungumzo hayo.
Kwanza ilianza kusikika sauti yangu nikisema, “Hello.”
Halafu ikafuatia sauti ya Shefa.
“Niko njiani, ninakuja.”
“Unakuja hapa nyumbani?”
“Ndiyo.”
“Subiri. Unajua watu wa hapa nyumbani hawajalala bado. Kwani huwezi kuja saa sita hivi?”
“Ninaweza.”
“Basi njoo muda huo. Nitaacha mlango wazi; ukija unaingia tu.”
“Sawa.”
Mawasiliano yakakatika hapo.
Nikainua uso wangu na kumtazama Raisa.
“Hapo pia utakataa kuwa Shefa hakuja kwako?” Raisa akaharakisha kuniuliza.
“Sitakataa, shoga. Ni kweli alikuja kwangu, lakini niliogopa kukubali kutokana na yale yaliyotokea.”
“Yaliyotokea pia yameshafahamika. Inasemekana Shefa ulilala naye hadi saa kumi usiku, mkaanza kugombana, ukachukua rungu ukampiga nalo. Usiku wa tatu ukamweka mwili wake kwenye gari na kwenda kuutupa makaburini. Nilikuona na nililiona gari lako, lakini ulikataa,”
Nikatikisa kichwa changu kwa kusikitika.
“Sijui kama utaniamini, shoga. Nilikuficha kwa sababu ya kujihami. Nilikuwa naogopa. Shefa ameuawa nyumbani kwangu. Shefa ana mke wake na mimi nina mume wangu. Kwa kweli nilifanya vile ili kuficha ile siri, lakini kama kila kitu kimeshafichuka nitakueleza ukweli, shoga yangu. Mimi sikumuua Shefa.”
“Shefa alikufa nyumbani kwako na mume wako alikuwa hayupo; utasema aliuawa na nani?”
Nikamueleza Raisa kilichotokea. Raisa hakutaka kukubali. Akaniambia nilikuwa ninaendelea kumficha ukweli.
“Ukweli ndio huo niliokueleza; niamini.”
“Sasa hata kama hukumuua Shefa, nani atakuamini?”
“Ndiyo hapo sasa, lakini sikumuua Shefa wala sina sababu ya kuua mtu.”
“Sasa nimesikia shoga unakuja kukamatwa nikaona nikujulishe, shoga yangu; usije ukakamatwa ghafla. Laiti ningejuwa tangu mwanzo tungeweza kushauriana na kujua tufanye nini.”
“Hata sasa tunaweza kushauriana.”
“Umechelewa. Usishangae kwamba hivi sasa polisi wako nyumbani kwako wanakutafuta.”
Nikanyamza kimya.
“Sasa sijui utakimbilia wapi?” Raisa akaniuliza.
“Nitakimbilia Dar.”
“Unataka kwenda Dar leo hii?”
“Nitaondoka kesho asubuhi.”
“Polisi watakukamata kabla hujaondoka.”
“Wataniona wapi?”
“Kwani hutarudi nyumbani kwako?”
“Sitarudi.”
“Utalala wapi?”
“Naweza kulala hata hapa kwako.”
Raisa akaguna.
“Lakini hutaniletea matatizo, shoga.”
“Matatizo ya nini?”
“Matatizo ya polisi. Wasije wakaona nimekuficha ili usikamatwe.”
“Sasa hao polisi watajuaje kama niko kwako, shoga yangu?”
Kabla Raisa hajajibu, simu yangu iliita. Nilishituka kidogo. Nikaona jina la mume wangu. Nikaipokea simu na kuamua kunyamza kimya.
“Uko wapi?” akaniuliza.
“Kuna nini, kwani?” nikamuuliza.
“Unatafutwa. Kuna watu wamekuja hapa nyumbani kukuulizia.”
“Ni kina nani?”
Sufiani akawa kimya kwa sekunde tatu, kisha akanijibu, “Njoo hapa nyumbani, atawaona.”
Nikajua wageni hao ni polisi waliokuja kunikamata. Sufiani alipokuwa kimya, walikuwa wakimwambia asiwataje.
“Mimi niko saluni, nina kazi,” nikamdanganya.
Sufiani akakata simu bila kuniambia chochote, lakini nilikuwa na imani kuwa polisi hao wangenifuata saluni.
Haukupita muda mrefu, baba naye akanipigia.
“Uko saluni?” akaniuliza.
“Ndiyo, niko saluni,” naye nikamdanganya.
“Polisi wamemchukua mume wako, wanakuja naye huko.”
“Mimi siko saluni, niko mahali pengine.”
Sikutaka kumwambia niko wapi kwani nilihisi anaweza kubanwa na polisi akawambia kuwa niko kwa Raisa.
Nikakata simu na kuizima kabisa.
“Raisa, unipe hifadhi hapa kwako hadi kesho niende Dar,” nikamwambia, uso wangu ukiwa umefadhaika.
“Mimi sina tatizo, shoga yangu. Utalala tu hapa hadi hapo kesho,” Raisa akaniambia.
“Yaani nimepata matatizo ambayo sikuyatarajia; hata sijui ni hayawani gani aliyemuua yule mtu na kuniachia kizaazaa hiki!”
“Saa hizi mwenzako amekaa mahali ametulia, balaa unalo wewe!”
“Mwenzagu! Hata sijui niseme nini…!”
Siku ile nilishinda kwa Raisa hadi usiku. Nilikula naye chakula ingawa sikula sana kwa sababu ya hofu ya kukamatwa. Akanibembeleza niendelee kula.
“Kula, shoga yangu, punguza mawazo,” akaniambia.
“Mh! Shoga… hicho kidogo nilichokula kinanitosha. Si kwamba nimeshiba, bali nimekinai.”
“Kwa nini sasa ukinai kula, shoga yangu, wakati nimepika chakula kingi kwa ajili yako?”
“Ni wasiwasi tu, shoga yangu.”
“Wasiwasi wa nini? Wewe umesema kesho asubuhi unaondoka kwenda Dar; sasa wasiwasi wako ni wa nini?”
“Kwani huko Dar haiwezekani kukamatwa?”
“Utajificha. Wangapi wamefanya uhalifu na wanatafutwa na polisi hadi leo hawajapatikana; miaka inaenda.”
“Sasa, bora hao ambao wamefanya uhalifu wametulia kwa sababu wamefanya walichokitaka. Na hata kama watakamatwa ni haki yao kwa sababu wamefanya makosa. Lakini mimi sikufanya kosa lolote. Hata kama sitakamatwa nitabaki na wasiwasi na uchungu siku zote.”
“Hukamatwi, shoga. Ila tu ukifika Dar nifahamishe mahali ulipo ili siku moja moja nikutembelee.”
“Nitakufahamisha, usijali. Wewe ni rafiki yangu.”
“Hili jambo litakwisha tu. Kama lilivyokuja bila hodi, litaondoka bila kwaheri.”