Chaumma yaahidi kujenga barabara ya Uvinza-Kasulu

Kigoma. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi kujenga barabara ya lami kutoka Uvinza hadi Kasulu Mjini kupitia Kata ya Basanza, endapo atachaguliwa kuwa Rais Oktoba 29, mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Septemba 20, 2025, katika Kata ya Basanza, Mwalimu amesema barabara hiyo ni muhimu kwa ajili ya kufungua fursa za kiuchumi kwa kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa, pamoja na kuunganisha jamii ya Kigoma Kusini na maeneo mengine ya nchi kwa ufanisi zaidi.

“Barabara ni uti wa mgongo wa maendeleo. Bila miundombinu bora, huwezi kuimarisha biashara, kilimo, elimu wala huduma za afya kwa ufanisi.

“Hii barabara ya Uvinza-Kasulu kupitia Basanza ni hitaji la muda mrefu, na tukipata dhamana, tutajenga kwa kiwango cha lami,” amesema Mwalimu huku akishangiliwa na wakazi wa eneo hilo.

Huku akizungumzia changamoto zinazowakabili wakazi wa Basanza na maeneo ya jirani, amesema barabara hiyo kwa sasa ni kikwazo kwa maendeleo, hasa nyakati za mvua ambapo huwa haipitiki, huku kipindi cha kiangazi ikikumbwa na vumbi zito, licha ya juhudi za kukwangua kwa greda.

“Tunaahidi si matengenezo ya muda mfupi, bali ujenzi wa kudumu wa lami unaozingatia viwango, kwa lengo la kuwezesha wakulima, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kusafiri kwa uhakika mwaka mzima,” amesema.

“Niwaahidi, niaminini msela mwenzenu. Nikichaguliwa kwenda ikulu, naenda kuwajengea barabara hii kwa kiwango cha lami ili shughuli za kiuchumi zifanyike na muepukane na adha mnayopitia,” amesema Mwalimu.

Ameahidi kuwa, ndani ya miaka miwili akiwa madarakani, Serikali yake itahakikisha ujenzi huo unakamilika, ili kuondoa adha hiyo kwa wananchi na kuwezesha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Ukiondoa vikwazo vya usafiri, mkulima wa kijijini anaweza kuuza mazao yake kama vile mawese au maharage kwa wakati, bila kuhofia kuozea njiani au kuchelewa kwa sababu ya mvua au ubovu wa barabara,” ameeleza.

Katika sera zake za maendeleo, Mwalimu ameweka msisitizo kwa sekta ya ulinzi na usalama, akiahidi kuwa Serikali ya Chaumma itawekeza kwa kiasi kikubwa katika teknolojia ya kisasa kwa vyombo vya dola, ikiwemo Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

“Katika dunia ya leo, huwezi kuwa salama kwa kutumia vifaa vilivyopitwa na wakati. Tutawekeza katika teknolojia ili vyombo vyetu vya ulinzi viwe vya kisasa, vya haraka na vya kuaminika na wananchi wajiwekee matumaini kuwa nchi yao iko mikononi salama,” alihitimisha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chaumma, John Mrema amesema wamemleta mgombea urais kijana mwenye uzoefu, akitaja kuwa Mwalimu alishawahi kuwa mgombea mwenza mwaka 2020 kupitia Chadema, hivyo ana uelewa wa changamoto na namna ya kuzitatua.

“Msitamzame umbo lake, sikilizeni sera zake. Mwalimu anakuja na madini ya kuisaidia Tanzania,” amesema.

Naye Eliah Mahwa, mgombea ubunge wa Chaumma Kigoma Kusini, amesema jimbo hilo limetelekezwa kwa muda mrefu, hasa kwenye huduma za afya, hali inayochangia ugumu wa maisha kwa wananchi na kwamba akichaguliwa ataleta maendeleo.