Babati. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimeahidi kuchukua hatua za haraka kurejesha bei ya zao la mbaazi hadi kufikia Sh3, 000 kwa kilo iwapo kitaingia madarakani, baada ya bei kushuka hadi kati ya Sh650 na Sh700 kwa kilo mkoani Manyara.
Chama hicho kimesema soko la zao la mbaazi ni kubwa, hasa katika mataifa kama India, hivyo ni lazima wakulima wa Tanzania wanufaike nalo ipasavyo.
Sambamba na hilo, chama hicho kimeahidi kufungua viwanda vya mbolea visivyo na kodi ili wakulima wapate pembejeo kwa bei nafuu.
Akizungumza Septemba 19, 2025, katika Kata ya Bonga na Soko Kuu la Babati Mjini, mgombea mwenza wa urais wa Chaumma, Devotha Minja amesema chama kimejipanga kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo, hususan mbolea, kwa bei nafuu kupitia viwanda visivyo na kodi.
Amesema pia kuwa chama hicho kitalinda masilahi ya wakulima kwa kuweka mazingira ya soko huria yenye bei ya haki na kuondoa mageti ya ushuru barabarani.
“Tunalenga kuhakikisha mkulima ananufaika kuanzia shambani hadi sokoni. Mbolea si bidhaa ya kifahari, bali ni haki ya kila mkulima,” alisema Minja.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Babati Mjini kwa tiketi ya Chaumma, Joseph Shayo amesema bei ya mbaazi imeporomoka isivyostahili kutoka Sh3, 000 kwa kilo miaka mitatu iliyopita hadi kati ya Sh650 hadi Sh700 kwa sasa.
“Hili haliwezekani. Tukisema kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi, basi hatuwezi kuwapuuza wakulima wetu. Tutahakikisha bei inarudi juu kama zamani,” amesema Shayo.
Shayo, ambaye ni mwendesha bodaboda, amesema atapigania masilahi ya vijana wanaofanya kazi ya bodaboda na bajaji, akiahidi kuanzisha mfuko maalumu wa bodaboda na bajaji ili kusaidia maendeleo yao.
Pia amesema atahakikisha wagonjwa wanafuatwa na magari ya wagonjwa bure kupitia mfuko wa jimbo.