DK.SAMIA ASISITIZA UCHAGUZI KUFANYIKA KWA AMANI NA UTULIVU, WANANCHI WAJITOKEZE KUPIGA KURA OKTOBA 29

 Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya  Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupigakura katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika  Oktoba 29,2025 na kwamba hakutakuwa na vurugu kwani vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kulinda amani.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa Visiwa Zanzibar leo Septemba 20,2025 katika Viwanja vya Gombani ya Kale Mkoa wa Kusini Pemba Dk.Samia ametumia nafasi hiyo kuendelea kuwahakikishia wananchi uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu.

“Katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, wapo baadhi ya watu wanatamani kuvuruga amani, hivyo nitoe mwito kwa wananchi kutokubali kuchokozeka. 

“Lakini niwahakikishie Oktoba 29 mwaka hakutakuwa na vurugu zozote .Wananchi  wanapaswa kujitokeza kwa wingi kutimiza takwa la kidemokrasia kuchagua viongozi wanaowataka.Msichokozeke, kuweni kama mimi mama yenu, dada yenu na bibi yenu. 

“Mimi ninachokozeka sana lakini sikubali kuchokozeka. Tusiende kuvunja amani ya nchi, tutunze amani na utulivu. Tunapochokozwa tusichokozeke.

“Tarehe 29 hakutakuwa na vurugu, vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vyema kulinda nchi na ninayezungumza hapa ni Amiri Jeshi Mkuu,”amesema Dk.Samia alipokuwa akizungumza kuhusu umuhimu wa kulinda amani katika kipindi cha uchaguzi mkuu.

Amesisitizakatika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali imejitahidi  kusimamia utulivu wa kisiasa na amani ambapo hakuna vurugu zozote zilizosikika.”Wenzetu wanayolalamikia hakuna lisilozungumzika.”

“Tutakaa tutazungumza, tusiende kuleta vurugu kuvunja amani kwa sababu hili halikufanyika. Tukapige kura, turudi nyumbani tusubiri matokeo,” amesema mgombea Urais Dk.Samia .

Pamoja na hayo Dk.Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa Serikali za CCM ni vitendo na siyo maneno na ndio maana yote yaliyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2020-2025 yametekelezwa na maendeleo yanaonekana katika sekta mbalimbali.

“Pemba kila kukicha imekuwa ikibadilika ikiwa ni matokeo ya miradi ya maendeleo inayoletwa kisiwani hapa.Serikali za CCM zinafanyakazi kwa vitendo na siyo blah..blah…kila nikija Pemba mambo yanaendelea kubadilika,”amesema Dk.Samia alipokuwa akizungumza na wananchi hao akihitimisha mikutano yake ya kampeni Zanzibar.

Ametaja baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa ni ujenzi wa Uwanja wa Ndege Pemba ambao utakuwa wenye hadhi ya kimataifa huku akifafanua uwanja huo baada ya kukamilika ndege kubwa za abiria na mizigo zitatua, hivyo kufungua zaidi uchumi.“Watalii na ndege za mizigo watafika moja kwa moja Pemba badala ya kutua unguja.”

Aidha amesema miradi mingine ni ujenzi wa barabara ya Chake chake – Mkoani ambao fedha zake zimeshapatikana.”Ujenzi  wa Bandari ya Shumba utarahisisha shughuli za uchukuzi baina ya Pemba na Mombasa hatua ambayo itaondoa changamoto ya usafiri.”

Ameongeza kwamba wakazi wa maeneo hayo watatumia boti za kisasa badala ya usafiri wa vidau ambavyo usalama wake ni mdogo.Amesema kisiwa hicho kimenufaika kupitia ujenzi wa shule za ghorofa ikiwemo eneo la Kojani.

Akieleza zaidi Dk.Samia Suluhu Hassan kutokana na maendeleo makubwa yaliyopatikana ndio maana wanaoujasiri wa kuomba ridhaa ya kuchaguliwa tena. 

“Tunaamini tumeweza kufanya makubwa, makubwa mengine zaidi tunaweza kuyafanya. Tupeni mitano mingine tufanye makubwa zaidi. Tunafanyakazi kustawisha maisha ya wananchi. Mtu akifanyakazi ipasavyo atapata ujira kisha kufanya maendeleo. Kazi na Utu maana yake ni kusonga mbele.”