Dodoma Jiji na leo tena

WAKATI timu nne kati ya tano zilizokuwa nyumbani zikianza kwa kuvuna pointi zikiwa nyumbani katika raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, Dodoma Jiji inarudi uwanjani katika mechi za ligi hiyo ikiwa ugenini kwa mara nyingine dhidi ya Tabora United (TRA United).

Mechi hiyo pekee kwa leo inachezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora, huku Dodoma ikitoka kupoteza kwa bao 1-0 mbele ya KMC mapema wiki hii jijini Dar es Salaam.

Katika mechi 5 za ufunguzi wa msimu huu, ni Fountain Gate ikiwa pekee iliyopasuka nyumbani, kwani KMC na Coastal Union zilishinda mechi zao, huku Namungo na Mashujaa zikilazimishwa sare dhidi ya Pamba Jiji na JKT Tanzania.

Fountain Gate ambayo msimu uliopita ilichapwa mechi nne kati ya tano za mwisho kabla ya play-offs iliyowaikoa isishuke daraja, ndio timu pekee iliyochemsha nyumbani baada ya kulala 1-0 dhidi ya Mbeya City

Ikiwa Tanzanite Kwaara, Babati mkoani Manyara, Fountain Gate ilichapwa kwa bao la penalti la Habib Kyombo.

Ikumbukwe Fountain Gate ilisalia Ligi Kuu Bara kupitia mchujo baada ya kumaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya 14, ikiwa na pointi 29, ilishinda mechi nane, sare tano na kupoteza 17, ilikuwa na uhakika wa ushindi kwenye mechi zake kwa asilimia 26.7.

Katika mchujo, ilibwagwa na Tanzania Prisons ikasalia kwa kuifunga Stand United kwa jumla ya mabao 5-1.

Katika mechi tano za raundi ya kwanza, ni KMC na Coastal Union ya Tanga ndizo ambazo zimeanza vizuri zaidi nyumbani kwa kushinda mechi zao kwa bao 1-0.

KMC ndio ilikuwa timu ya kwanza msimu huu wa ligi kuibuka na ushindi baada ya kuilaza bao 1-0 Dodoma Jiji ambayo leo, Jumamosi ya Septemba 20 itacheza mechi yake ya raundi ya pili ugenini dhidi ya Tabora United.

Darueshi Saliboko ndiye aliyeamua mechi hiyo na kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la Ligi Kuu msimu huu huku Coastal nayo ikaendeleza ubabe wake dhidi ya Tanzania Prisons kwa kuichapa bao 1-0. Ikiwa nyumbani kama hivi msimu uliopita, Coastal iliichapa pia Prisons mabao 2-1.

Mechi nyingine ambazo zilichezwa juzi, Alhamisi zilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mashujaa na JKT Tanzania walitoka sare ya tatu mfululizo baada ya wababe hawa wa jeshi kutoka sare katika mechi zote mbili za ligi za msimu uliopita.

Cha kuvutia katika mechi ya kusini mwa Tanzania ambapo Namungo ikiwa Ruangwa dhidi ya Pamba, lilifungwa bao la mapema zaidi hadi sasa na Shafani Siwa aliyeitanguliza Pamba katika dk20 kabla ya mwenyeji kuchomoa katika dakika za jioni kabisa (90+6) kupitia kwa Abdulaziz Shahame ‘Haaland’.

Kwa mechi ambayo itapigwa leo, kati ya Tabora United dhidi ya Dodoma Jiji, rekodi inaonyesha wote hakuna aliyeshinda hata mmoja katika mechi zake tano za mwisho.