Dar es Salaam. Ilikuwa siku ya furaha, lakini tukio la Steven Mabula, kupiga goti mbele ya Marietha Lazaro alipomvisha pete ya uchumba, lilitia doa hafla hiyo.
Wapo walioelewa ishara ya tukio hilo, lakini haikuwa hivyo kwa baba wa Steven. Aliamini kijana wake amekiuka misingi ya mila na desturi.
“Nilipiga goti bila kufahamu ishara hiyo ina maana gani zaidi ya kuona kwenye matukio ya baadhi ya watu,” anasema.
Anasema baba yake hakumwelewa, alimuona kuwa amefanya jambo lisilostahili, kwani aliyepaswa kupiga goti ni mwanamke.
“Baba alisusa hakuja harusini, aliona nimedhalilisha mila zetu, kwa mwanamume kumpigia goti mwanamke,” anasema.
Kwa upande wake, Alfani Mahamoud anasema siku alipomvisha pete mchumba wake aliambiwa apige goti.
“Nilikataa, nikamwambia mke wangu (Salma, ambaye alifunga naye ndoa Januari 31, 2025), wewe ndiye unatakiwa upige goti,” anasema na kuongeza:
“Alitii akafanya hivyo, lakini baadhi ya rafiki zangu walinisema kwa kitendo kile, wakiamini mwanamume ndiye anapaswa kumpigia goti mwanamke wakati wa kumvisha pete ya uchumba.”
Wawili hao ni miongoni mwa wengi wanaopiga goti pasipo kujua undani wa tukio hilo, huku swali likiwa nani anastahili kupiga goti, mwanamke au mwanamume?
Kiongozi wa kimila kutoka Kanda ya Ziwa, Nyang’wale Matutu anasema jamii nyingi katika miaka ya nyuma hazikuwa na utaratibu wa uvishanaji pete za uchumba.
“Kijana akitaka kuchumbia wanatumwa watu wazima kwenda kuzungumza na familia ya binti, zitapelekwa zawadi ambazo sasa tunaita mahari, binti ataolewa. Hivi sasa ‘uzungu’ mwingi, watu wanachumbiana kwa mbwembwe, watavishana pete na mambo kama hayo ambayo si asili yetu,” anasema.
Anatoa mfano wa jamii, hususani za Kanda ya Ziwa, kuwa mwanamume kumpigia goti mwanamke ni mwiko.
“Lakini utandawazi leo hii unatubadilisha, tunaona wanawake wanapigiwa magoti wakiwa wanachumbiwa, jambo ambalo zamani halikuwapo, na si zamani tu, hadi sasa kuna jamii bado hazikubaliani na kitu hicho,” anasema.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi Mashariki na Pwani, Daniel Sendoro anasema watu kuchumbiana na kuvishana pete si jambo la protokali (halina utaratibu maalumu, kanuni au kisheria).
“Si maagano ya kidini, kwa sababu uchumba watu wanaruhusiwa kuahirisha, hiyo si ndoa, japo kwa mapokeo ya kisasa familia zingine huwa zinahusisha viongozi wa dini ili kuwaombea katika mpango huo,” anasema na kufafanua:
“Lakini hilo si jambo la viapo vya kikuhani, huwa linahusisha viongozi wa dini kama familia zitataka, ili kuliombea jambo hilo la heri liweze kufanikiwa.”
Anasema uchumba unaweza kuvunjika kwa sababu mbalimbali, mtu hawezi kulalamika eti mchumba amemuacha kwani huo ni urafiki ambao unakomazwa kuwa ajenda ya viapo vya mke na mume baadaye.
Kuhusu nani anayestahili kumpigia goti mwenzake wakati wa kuvalishana pete ya uchumba, Mchungaji Sendoro ambaye pia ni mwanasaikolojia anasema magoti ni ishara ya unyenyekevu na utii.
“Kisosholojia mwanamume anapompigia goti mwanamke, kuna vitu viwili vinatokea, kwanza ni tangazo la uaminifu kwa huyo anayempigia goti. Jambo la pili ni la kijamii ambalo ni baya pale mwanamume anapompigia goti mwanamke, anaondoa ule utawala na utii anaostahili kupewa na mwanamke,” anasema.
Anasema hata asili inabainisha mke kumtii mume, akifafanua kuwa si jambo sahihi kwa namna yoyote ya kiroho, kijamii na kisaikolojia mwanamume kumpigia goti mwanamke.
“Ishara hiyo inayoonekana nje inadhihirisha ndani kwamba, huyo mwanamume ataendelea kumpigia goti mwanamke, jambo ambalo hata nature (asili) inakataa.
“Mwanamume ni kiongozi, ni kichwa cha familia, hata kiroho ipo hivyo, anapaswa kuwajibika kama mume, anaposhindwa kuwajibika ndipo tunaona haya ya kumpigia goti mwanamke,” anasema.
Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waisalmu Tanzania (Bakwata), Alhaji Nuhu Mruma, anasema pete ya uchumba ni utamaduni wa kigeni ambao haupo katika imani ya Kiislamu.
“Wengi wanafanya hivyo ili kutengeneza utambulisho kwa jamii kwamba fulani ni mchumba wa mtu, lakini katika dini siyo lazima,” anasema.
Anasema ikitokea wanaochumbiana wakata kiongozi wa dini kushiriki ili kuwaombea heri, hilo hufanyika lakini halipo katika imani ya dini kwamba mtu anapochumbiwa basi avalishwe pete ya uchumba.
Kuhusu mwanamume kupiga goti anasema kitendo hicho hakipo, kwani yeye ndiye kichwa cha familia na ndiye kila kitu, kauli inayoungwa mkono na Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhani Kitogo.
“Labda nje ya Uislamu, lakini katika imani yetu mwanamume kumpigia mwanamke goti haipo, hii ndiyo inasababisha mtu kumwita mkewe mama. Unapompigia goti unakuwa kama unaungama kwake, ni kujidhalilisha na kujishusha pamoja na kula kiapo cha utiifu kwake, wakati mwanamume ndiye anapaswa mkewe amtii,” anasema.
Sheikh Kitogo anasema: “Katika dini yetu kumchumbia mwanamke ni kutoa taarifa kwao na kufuata taratibu za kifamilia, huo ndio msingi wa kuchumbia, hayo mengine ya pete ni wenyewe tu, lakini hayahusiani na dini.”
Katibu Mtendaji Idara ya Liturujia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Clement Kihiyo amesema upigaji goti ni ishara ya kumuomba mwanamke kutoka kwao na kuingia kwenye familia ya mwanamume.
“Hii haimaanishi huyo mwanamume ni mdogo kwa mwanamke anayempigia goti, la hasha, bali ile ni ishara ya heshima ya kumuomba kutoka kwenye familia yake, na kuingia kwenye familia ya mume wake mtarajiwa,” anasema.
Philimon James, mzee wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Bonyokwa mkoani Dar es Salaam, anasema katika imani ya madhehebu hayo hakuna tukio la pete, ingawa mtu anaweza kufanya nje ya kanisa akitaka.
Upigaji goti (hasa moja) kwa mujibu wa mitandao ya kijamii chanzo chake ni mchanganyiko wa mila za Ulaya, dini na maadili ya kifalme.
Inaelezwa katika zama za kati (karne ya 11–15), wapiganaji (knights) wa Ulaya walipiga goti moja mbele ya mfalme au bwana wao kama ishara ya heshima, utiifu na uaminifu. Ishara hiyo ilihusishwa na heshima na kuonyesha unyenyekevu.
Baadaye, ikaingizwa kwenye mapenzi kwamba, mwanamume akipiga goti mbele ya mpenzi wake wakati wa uchumba anaashiria heshima na uaminifu uleule wa mpiganaji.
Inaelezwa kwa dini za Kikristo, kupiga magoti ni ishara ya maombi, heshima na ibada mbele ya Mungu, hivyo ukifanyika mbele ya mtu unayempenda, hufananishwa na zawadi ya kiroho.
Si hivyo tu, inaelezwa katika ndoa Ulaya, mchumba aliyepiga goti alionekana kuonyesha kujitoa kwake na kumweka mwanamke katika nafasi ya heshima.
Kwa mujibu wa Wikipedia, Karne ya 13 Ulaya kulikuwa na kumbukumbu kwenye mashairi ya courtly love (mapenzi ya kifalme), ikielezwa mwanamume akipiga goti mbele ya mwanamke na kumpa zawadi kama ishara ya mapenzi.
Sir Walter Scott (katika miaka ya 1800, Uingereza) katika riwaya zake, kuna maelezo ya wanaume kupiga goti kuomba kuchumbia, yakichora picha ya heshima na unyenyekevu.
Vilevile, Malkia Victoria na Prince Albert (miaka ya 1840, Uingereza) ingawa haijathibitishwa kwa picha, ripoti zinaeleza Prince Albert alitumia desturi ya kupiga goti alipomvisha Victoria pete, jambo lililoeneza zaidi mtindo huo miongoni mwa tabaka la kifalme.
Hivi sasa filamu na tamthiliya za mapenzi huonyesha mwanamume akipiga goti moja wakati wa uvishanaji pete ya uchumba, jambo lililoeneza mtindo huu duniani.
Kwa mujibu wa mtandao wa kampuni ya vito ya Baunat ya mjini Antwerp, nchini Ubelgiji, ndoa katika jadi ya Kiafrika zilitofautiana kwa mujibu wa mila, tamaduni na desturi lakini hazikuhusisha uvalishanaji wa pete.
Tovuti ya Makumbusho ya Almasi ya Jiji la Cape Town, Afrika Kusini, inaeleza kubadilishana pete kati ya watu wawili kulifanyika kwa mara ya kwanza Misri ya Kale. Maandishi yanayojulikana maandiko ya papyrus, yalionyesha wanandoa wakibadilishana pete zilizotengenezwa kwa nyuzi au mianzi.
Pete hizo hazikudumu muda mrefu, zilibadilishwa kwa zile za ngozi au pembe ya ndovu. Kadri malighafi ilivyokuwa ghali zaidi, ndivyo upendo ulivyoonyeshwa kwa yule anayepokea pete hiyo. Zaidi ya hayo, aina ya malighafi pia iliwakilisha thamani ya mali ya anayetoa pete.
Inaelezwa pete ziliwakilisha upendo wa milele na kujitoa kati ya watu wawili, duara la pete likiwakilisha kutokuwa na mwanzo wala mwisho. Ndani ya pete liliwakilisha siku za usoni.
Kwa mujibu wa mtandao huo, katika Roma ya Kale, bwana harusi alimvisha mchumba wake pete ya chuma. Hivyo kuwa mwanzo wa kutumia metali za thamani katika pete za ndoa hadi leo. Metali yenye kudumu iliwakilisha uimara na nguvu, ishara ya uhusiano wa wanandoa.
Kwa mujibu wa mtandao huo, Warumi ndio wa kwanza kuandika maandishi kwenye pete za metali na kwamba, wao na Wagiriki, walivaa pete kidole cha nne mkono wa kushoto kama ilivyo leo. Kidole cha pete kiliaminika kuwa na mshipa unaoelekea moja kwa moja kwenye moyo.