ZIKIWA zimesalia siku tano kabla ya kucheza dhidi ya Simba, Fountain Gate imeiandikia barua Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuomba mchezo huo usogezwe mbele.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara, umepangwa kuchezwa Septemba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo kwa Simba utakuwa wa kwanza msimu huu wakati Fountain Gate kwao ni wa pili baada ya kuanza kufungwa 1-0 na Mbeya City, Septemba 18, 2025.
Taarifa iliyotolewa leo Septemba 20, 2025 na uongozi wa Fountain Gate, imeeleza sababu za kuiandikia TPLB kuomba mechi zake zijazo kusogezwa mbele ni kutokana na changamoto waliyokumbana nayo katika mfumo wa usajili.
“Uongozi wa Fountain Gate FC unapenda kutoa ufafanuzi kuhusu changamoto zilizojitokeza katika mchezo wetu wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, Septemba 18, 2025.
“Kikosi chetu kililazimika kushuka dimbani kikiwa na wachezaji wachache kutokana na tatizo la kiufundi katika mfumo wa usajili wa kimataifa (TMS), licha ya taratibu zote za usajili kukamilika kwa wachezaji wetu wapya.
“Changamoto hii ilitokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa klabu na tayari juhudi za pamoja kati ya Fountain Gate FC na TFF zinaendelea kutafuta suluhisho la kudumu.
“Hali hii imeathiri maandalizi ya timu, kwani kwa sasa tuna idadi ndogo ya wachezaji waliothibitishwa kucheza, huku baadhi wakikabiliwa na changamoto za kiafya na majeraha. Kutokana na hali hiyo, tumeiandikia Bodi ya Ligi (TPLB) kuomba michezo yetu isogezwe mbele mpaka pale suluhisho na mwafaka wa changamoto hii utakapopatikana.
“Fountain Gate FC inatambua umuhimu wa ushindani wenye uwiano katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Tunaamini Kwa kushirikiana na TFF na TPLB tutaweza kupata mwafaka wa haraka, na kuruhusu timu yetu kushiriki ligi kwa kikosi kamili na chenye ushindani.
Tunawaomba wadau wetu wote kuendelea kuwa na subira na kuipa timu yetu sapoti wakati huu wa mpito,” ilieleza taarifa hiyo.
Katika mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City ambao Fountain Gate ilikuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, kikosi hicho kilikuwa na wachezaji 11 walioanza huku watatu wakikaa benchi.