Ligi Kuu Zanzibar njiapanda, klabu, Bodi ya Ligi zatofautiana

BAADA ya Septemba 14, 2025 kuchezwa Ngao ya Jamii kati ya KMKM dhidi ya Mlandege ikiashiria kufunguliwa kwa msimu wa 2025-2026, huku Ligi Kuu Soka Zanzibar (ZPL) ikitarajiwa kuanza leo Septemba 20, 2025 kwa kuchezwa mechi moja, kuna sintofahamu imejitokeza juu ya uwepo wa mchezo huo.

Kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) na ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi Zanzibar, inaonesha ligi hiyo inaanza leo Septemba 20, 2025 kwa mchezo kati ya Polisi dhidi ya Uhamiaji uliopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja, saa 10:15 jioni.

Katika ratiba hiyo, raundi ya kwanza inaonesha itakuwa na mechi nane, huku KMKM na Mlandege zikishuka dimbani Oktoba 3, 2025 baada ya kukamilisha mechi zao za kimataifa hatua ya awali. Kumbuka Mlandege inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na KMKM ipo Kombe la Shirikisho Afrika.

Wakati ikiwa hivyo, taarifa zinabainisha ligi hiyo imepelekwa mbele hadi Septemba 25, mwaka huu, huku sababu ikitajwa ni kuwepo kwa mchakato wa kumpata Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Zanzibar.

Mwanaspoti lilipomtafuta Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Zanzibar, Issa Kassim kuhusiana na taarifa za kusogezwa mbele ligi hiyo kutokana na uwepo wa mchakato wa uchaguzi huo, amesema: “Sio kweli, ligi itaendelea kama kawaida, hivyo ni vitu viwili tofauti.”

Wakati kiongozi huyo akisema hayo, uongozi wa timu ya Polisi umesema umepokea taarifa ya kutokuwepo kwa mchezo wao leo dhidi ya Uhamiaji. 

Kwa upande wa timu ya Uhamiaji, imesema katibu wa timu hiyo alikwenda katika ofisi ZFF na kuambiwa ligi hiyo inatarajiwa kuanza Septemba 25, 2025 badala ya Septemba 20, mwaka huu.

“Mpaka sasa ZFF haijatuma ratiba kwa klabu yoyote kwamba ligi hiyo inatakiwa kuchezwa, katibu wetu alikwenda kuulizia akaambiwa inatarajiwa kuanza Septemba 25,” amesema kiongozi mmoja wa Uhamiaji.

Septemba 3, mwaka huu, ZFF lilitoa taarifa ya uchaguzi mdogo kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi na Mjumbe anayewakilisha klabu kutoka Ligi ya Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja, uchaguzi huo ulifanyika kufuatia Mwenyekiti aliyekuwepo, Suleiman Salum Suleiman timu yake kushushuka daraja na kupoteza sifa ya kuendelea kushika nafasi hiyo.

Uchaguzi huo uliofanyika Septemba 16 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Chuo cha Mafunzo kisiwani hapa, haukutoa mshindi baada ya kura kupigwa mara mbili huku matokeo yakiwa sare jambo ambalo lilisababisha Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Mussa Hamad Tajo kuahirisha uchaguzi huo.

“Naahirisha uchaguzi kwa mujibu wa kifungu cha 13 cha kanuni za uchaguzi baada ya kujiridhisha,” alisema Tajo.

Wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti katika uchaguzi huo ni Hussein Ali Ahmada na Haji Issa Kidali. Baada ya kuahirishwa, Kidali alionekana kushangazwa na uamuzi huo lakini hakuwa na budi kukubali huku Ahmada akisema hadi kufikia sasa hawajapokea taarifa yoyote inayohusu kurudiwa kwa uchaguzi huo.