Tanga. Mgombea udiwani wa Kata ya Msambweni, jijini Tanga kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Bakari Idd Chuo ameahidi kutafuta njia mbadala ya kupata mikopo nafuu kwa wananchi wake na kuepukana na ile ya “kausha damu,” ambayo imesababisha baadhi ya ndoa kuvunjika.
Akizungumza katika kampeni zake za kujinadi zilizofanyika maeneo ya Tamta, Kata ya Msambweni, jijini Tanga, leo, Jumamosi, Septemba 20, 2025, mgombea huyo amesema mikopo umiza imekuwa changamoto kubwa kwenye familia nyingi.
Amesema akipewa ridhaa na wananchi na kumchagua kuwa diwani wao Oktoba 29, 2025, atatafuta njia mbadala ya wananchi wake kupata mikopo, badala ya ile hali ya sasa.
Ameongeza kuwa katika halmashauri kuna mikopo ya asilimia 10 inayotakiwa kwenda kwa wanawake, vijana, na wenye ulemavu, ila usimamizi wake ndio changamoto. Hivyo, ameahidi kuwa atakwenda kusimamia watu wa kata ya Msambweni wenye sifa ili waweze kupata mikopo.
Pia, ameahidi kwenda kutatua changamoto za barabara za mitaa zilizopo katika kata yake na kueleza kuwa nyingi hazina ubora na hazijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu, hivyo akipewa ridhaa atakwenda kuzifanyia kazi.
Ahadi nyingine ni kuhusu ukosefu wa zahanati katika kata hii, ambapo amesema iwapo atapewa ridhaa, atahakikisha anajenga zahanati ya kata ili wananchi wapate huduma za afya karibu na kwa wakati.
“Kwenye suala hili, nitahakikisha tunapata zahanati yenye viwango bora, ambapo wajawazito, watoto, na wananchi wengine wanapata huduma karibu kabla ya kwenda hospitali kubwa.
“Eneo letu lina taasisi za vyuo vya Kiislam viwili na shule ya msingi, kuna watoto zaidi ya 600, ikitokea dharura ni hatari,” amesema Bakari.
Kwa upande wake, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zaina Mahanyu, amesema kuwa katika Jimbo la Tanga Mjini, chama hicho kimesimamisha wagombea udiwani katika kata zote 27, na hivyo kuwaomba wananchi kuwapa kura za ndiyo ili kuleta mabadiliko ya kweli kutoka ngazi ya chini kabisa ya uongozi.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni, Zaina amesisitiza kuwa uchaguzi huu ni fursa ya kipekee kwa wananchi wa Tanga kuchagua viongozi wanaojali maslahi yao, na kwamba amani na haki ni misingi muhimu ya mchakato huo.
“Tukisisitiza amani na haki katika uchaguzi, wananchi watajitokeza kwa wingi kupiga kura bila woga. Tunaviomba vyombo vya dola visaidie kulinda misingi hiyo, ili kila Mtanzania awe huru kuchagua kiongozi anayemtaka,” amesema Zaina.
Ameeleza kuwa ACT-Wazalendo inalenga kuboresha sheria ndogo ndogo na kushinikiza mabadiliko ya sera zitakazowanufaisha wananchi moja kwa moja, hususan katika maeneo ya mikopo, biashara ndogondogo, na kodi zisizokuwa rafiki.
“Mazingira ya jiji la Tanga bado yanahitaji maboresho makubwa. Tukipata madiwani wetu katika kata zote, pamoja na mbunge wetu Seif Abal Hassan, tutahakikisha sauti za wananchi zinasikika na changamoto zao kushughulikiwa,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa ACT-Wazalendo Kata ya Msambweni, Mwajadi Rashid Salim, alipomnadi mgombea wa udiwani wa chama hicho, amewahakikishia wananchi kuwa chama kimechagua wagombea waadilifu, waaminifu, na wenye maono, na iwapo watakiuka maadili au kushindwa kutekeleza ahadi zao, watawajibishwa na chama.
“Tuwachague viongozi wanaotuelewa, wanaotoka miongoni mwetu, na wenye dhamira ya kweli. Huu ni wakati wa kufanya maamuzi sahihi. Kura yako ni silaha ya mabadiliko,” amesema Mwajadi.
Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo, akisisitiza kuwa ni haki yao ya msingi kuchagua viongozi wanaowatetea na kuwatumikia kwa uaminifu.