MO aweka pesa Coastal Union

COASTAL Union ya Tanga, mapema leo imeingia makubaliano ya mkataba wa mwaka mmoja na kampuni ya Mo Taifa kama mdhamini wa timu hiyo.

Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari, Mkurugenzi wa Masoko ya kampuni hiyo, Fatema Dewji amesema sababu ya kuidhamini Coastal ni pamoja na ubora na ushindani unaoendelea kuonyeshwa na timu hiyo katika Ligi Kuu Bara.

“Nina furaha kubwa ya kutangaza kuingia makubaliano na Coastal, ni kielezo cha kweli kwamba tunagusa maisha ya watu na sio Coastal Union pekee, naamini udhamini huu utakuwa na manufaa kwa Wana Tanga.

“Udhamini utakuwa wa mwaka mmoja 2025/26 lengo ni kuwawezesha mashabiki na jamii, tunatarajia msimu wenye mafanikio makubwa kwa sababu Coastal ni timu nzuri,” amesema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Coastal Union, Hassan Hussein, amesema udhamini huo utaongeza chachu msimu huu kwani kushiriki Ligi Kuu bila ya udhamini ni changamoto kubwa.

“Bila ya kuwa na udhamini kwa timu zetu hizi itakuwa ngumu kidogo, sisi na kampuni ya Mo tuna ushirikiano mzuri tangu Ligi Daraja la Kwanza, wamekuwa na sisi hadi tukapanda Ligi Kuu walitushika mkono.

“Tunaamini udhamini huo utasaidia kuibua vipaji vya vijana wengi kwani pesa inapowekwa kwenye timu hata wachezaji wanaonyesha viwango vyao na kujituma zaidi,” amesema.