Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman ameeleza namna Serikali itakayoundwa na chama hicho, itakavyowawezesha Wazanzibari kujikwamua kiuchumi.
Amesema ACT-Wazalendo, ina mipango lukuki ya kuwawezesha Wazanzibari ikiwemo kuwasaidia wananchi wenye kipato duni au wasiokuwa na njia ya kujipatia kipato.
“Hawa ndio wale waliokuwa wamekaa tu au kugalagala bila kuwa na njia ya kupata kipato. Ni wajibu wa Serikali kumsaidia mwananchi, hiki ndicho tutakachoenda kukifanya,” amesema Othman.
Othman ameeleza hayo leo Jumamosi Septemba 20, 2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kunadi sera zake uliofanyika uwanja wa Zantex, Jimbo la Mpendae mkoa wa Mjini Magharibi.
Mgombea huyo, ameendelea na mikutano yake ya hadhara Mjini Unguja baada ya kukamilisha kampeni hizo kisiwani Pemba kwa awamu ya kwanza.
Othman amefafanua kuwa jambo la kwanza litakalofanywa na ACT-Wazalendo ni kuwatambua, kisha kuwawezesha lile wanaloliweza, kwa kuwapa maarifa yatakayowawezesha kujiajiri.
“Mpango huu utakuwa na mfuko wake na utaratibu wake kwa sababu watu wasiojiweza au kutojua wafanye nini wapo. Kazi ya Serikali au chombo kitakachosimamia jambo hili ni kumwambia wewe unaweza kufanya hili, au tunampa mtaji,” amesema.
Othman amesema jambo jingine ni kuwawezesha wale wananchi wenye uwezo kidogo ili kusonga mbele zaidi, akisema kundi hilo ni muhimu kwa sababu watashika mkono wengine wasiojiweza.
“Tutawezesha maarifa na vifaa vya kisasa ili kuzalisha vizuri hasa mafundi fenicha. Watu wa namna hii ni kuwapatia mashine za kisasa na zipo kwa bei rahisi, kikubwa ni kupatiwa maarifa ya namna ya kuzitumia,” amesema Othman.
Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema hataki kuwadanganya wananchi wa kisiwa hicho, kwamba Serikali itawaajiri bali ajira itakayokuwepo ni kuwatengenezea mpango utakaowasaidia kujiajiri.
“Mpango huu tumeshautayarisha na tutauzindua siku maalumu baada ya kuunda Serikali Oktoba, nataka muone namna Zanzibar itakavyokuwa na neema. Lakini kazi yenu ndogo tu, ili tufanikiwe kura zenu leteni kwa OMO,” amesema Othman huku akishangiliwa.
Katibu wa Uenezi, Habari na Mawasiliano kwa Umma wa ACT Wazalendo, Salim Biman amesema wanachama wa chama hicho na wananchi, waliohudhuria mkutano huo wanatoka katika majimbo matatu ya mkoa wa Mjini Magharibi.
“Kesho tutakuwa jimbo la Kijini Kaskazini Unguja, wakati Jumatatu Septemba 22, tutakuwa Tomondo na siku inayofuata tutafanya mkutano Jimbo la Bububu,” amesema Biman.