KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua jioni ya jana alikuwa Angola kucheza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete Banguela, lakini mapema alitoa kauli ya kibabe kwa timu pinzani zitakazokutana na wababe hao wa Tanzania katika michuano yote.
Nyota huyo aliyeifunga Simba kwa mara ya tatu katika mashindano tofauti, alisema kwa kikosi kilichopo Jangwani anaamini kina uwezo wa kubeba ubingwa wa michuano yoyote wakikaza buti.
Pacome anayeitumikia Yanga kwa msimu wa tatu sasa, akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, amekuwa na rekodi nzuri ya kufunga mabao 19 na asisti 14 katika misimu miwili iliyopita ya Ligi Kuu, aliliambia Mwanaspoti kuwa, msimu huu Yanga ina kikosi kipana kitakachowapa mafanikio ndani na nje ya Tanzania.
“Hata kocha tuliyenaye ni mzuri, anayetaka soka la ushindi kushambulia hasa wakati tunapokuwa na mpira, bila kusahau nidhamu wakati hatuna mpira,” alisema Pacome aliyekuwa akitajwa kama Mchezaji Bora wa Mwaka, japo tuzo hizo za msimu uliopita ziliota mbawa kimya kimya.
“Ni ngumu kukosa mataji msimu huu kutokana na ubora tulionao, licha ya kwamba wapinzani wetu nao wamejipanga vilivyo, lakini bado tunajiamini kwamba tuna uwezo wa kubadilisha mchezo wakati wowote.”
Kuhusu mipango aliyonayo msimu huu, Pacome alisema; “Licha ya kuanza vyema kwa kuifunga Simba lakini hainifanyi kujiona bora, bado napambana kuhakikisha malengo ya timu yanatimia. Naamini Mungu atasaidia utakuwa msimu mzuri kwa timu na kwangu pia, kwa sababu tumeanza vyema ili tusimuangushe kocha kwa kufanya anayotuelekeza.”