Simba, Azam, Singida BS zaweka rekodi ugenini CAF

ILICHOFANYA Yanga jana Ijumaa ikiwa ugenini nchini Angola baada ya kushinda mabao 0-3 dhidi ya Wiliete Benguela, ndicho kilichofanywa na wawakilishi wengine watatu wa Tanzania Bara katika michuano ya CAF, Simba, Azam na Singida Black Stars baada ya zote kupata ushindi leo.

Hiyo inaonesha ni mwanzo mzuri wa wawakilishi wetu katika michuano ya kimataifa msimu huu ambapo sasa inasubiriwa marudiano wikiendi ijayo kuona nani atafuzu hatua inayofuata kuisaka ile ya makundi.

Katika michezo hiyo iliyofanyika leo Septemba 20, 2025 katika nchi tofauti, wawakilishi hao wameweka rekodi ya kupata ushindi bila ya kuruhusu nyavu zao kutikiswa, ikiwa ni mara ya kwanza kutokea Tanzania timu zake zote zinazoshiriki michuano ya CAF kuanzia ugenini na kupata ushindi wa aina hiyo.

GABORONE UNITED 0-1 SIMBA
Bao pekee la Elie Mpanzu Kibisawala alilofunga kwa kichwa dakika ya 16 akiunganisha krosi ya nahodha, Shomari Kapombe, limeipa Simba ushindi wa 0-1 ikiwa ugenini nchini Botswana.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Obed Itani Chilume uliopo Francistown nchini Botswana, Simba imekuwa na mwanzo mzuri katika hatua ya awali ya michuano hiyo.

Kabla ya kuingia kwa bao hilo, Simba ilionekana kupanga mashambulizi ambayo yalitibuliwa na Gaborone United.

Hata hivyo, dakika ya 67, kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola alionyeshwa kadi nyekundu na kulazimika kutolewa katika benchi kufuatia.

Simba iliingia katika mchezo huo bila ya kiungo wake mkabaji, Yusuph Kagoma anayeitumikia kadi nyekundu aliyooneshwa msimu uliopita katika fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Ushindi huo ni mwendelezo wa rekodi bora kwa Simba inapokuwa nchini Botswana kwani mara nne zote ilipocheza hapo katika michuano ya CAF haijapoteza, ikishinda tatu na sare moja.

Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2003, ilipokutana na BDF XI katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikashinda 1-3, kisha ikafuzu hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 4-1.

Mwaka 2021, Simba ilipambana na Jwaneng Galaxy katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ugenini ilishinda 2-0, lakini nyumbani ikafungwa 1-3, ikatolewa mashindanoni kwa bao la ugenini wakati matokeo yakiwa 3-3.

Baada ya hapo, mwaka 2024, Simba ilipokutana tena na Jwaneng Galaxy katika hatua ya makundi, ugenini zilitoka 0-0, ikaja kushinda nyumbani kwa mabao 6-0.

Simba na Gaborone United zinatarajiwa kurudiana Septemba 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar ambapo mshindi wa jumla atafuzu hatua inayofuata kucheza na mshindi kati ya Simba Bhora ya Zimbabwe na Nsingizini Hotspurs kutoka Eswatini.

AL MERREIKH BENTIU 0-2 AZAM
Kocha Florent Ibenge ameanza vizuri kibarua chake katika Kombe la Shirikisho Afrika akiiongoza Azam kupata ushindi wa mabao 0-2 dhidi ya Al Merreikh Bentiu ugenini nchini Sudan Kusini kwenye Uwanja wa Juba.

Mabao ya Feisal Salum dakika ya 45 na Jephte Kitambala dakika ya 68, yameipa mwanga Azam katika kuisaka rekodi mpya ya kucheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF mwa mara ya kwanza.

Rekodi zinaonesha mara zote Azam iliposhiriki mashindano ya CAF, haijawahi kucheza hatua ya makundi ambapo sasa Ibenge ana kazi ya kufanya na kikosi hicho.

Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Septemba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar ambapo mshindi wa jumla anakwenda kucheza hatua inayofuata dhidi ya mshindi kati ya AS Port ya Djibouti na KMKM kutoka Zanzibar.

RAYON SPORTS 0-1 SINGIDA BLACK STARS
Kwa mara ya kwanza, Singida Black Stars ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika, imepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rayon Sports kwenye Uwanja wa Kigali Pele nchini Rwanda.

Marouf Tchakei ndiye aliyewapa tabasamu mabingwa hao wa Kombe ka Kagame 2025 baada ya kufunga bao pekee dakika ya 20.

Singida Black Stars inayofundishwa na Miguel Gamondi, kazi bado haijaisha, kwani kuna mchezo wa marudiano utakaofanyika Septemba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar. Mshindi wa jumla anacheza dhidi ya mshindi kati ya Flambeau du Centre ya Burundi na Al Akhdar ya Libya. 

ETHIOPIAN INSURANCE 2-0 MLANDEGE
Wakati wawakilishi wa Tanzania Bara wakianza vyema kwa kushinda mechi zao za ugenini, upande wa Mlandege ya Zanzibar, imekubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Ethiopian Insurance.

Mchezo huu uliofanyika leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Abebe Bikila, Adis Ababa, wenyeji walifunga mabao hayo kila kipindi na kuwapa nafasi ya kutamba kifua mbele kuelekea mchezo wa marudiano utakaofanyika Septemba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar ambapo mshindi wa jumla anakwenda kukabiliana dhidi ya mshindi kati ya APR ya Rwanda na Pyramids kutoka Misri.