MSHAMBULIAJI wa Simba, Jonathan Sowah usiku wa leo Jumamosi atakuwa bize uwanjani na kikosi cha timu hiyo katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana, huku akitema cheche mapema kwa msimu huu wa 2025-2026.
Nyota huyo wa zamani wa Mediama ya Ghana na Singida Black Stars, amejiwekea malengo ya kuvunja rekodi binafsi ya msimu uliopita aliyoiweka akiwa na Singida, huku akigusia ile ya mfungaji wa mabao mengi kwa msimu mmoja iliyowekwa na Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ mwaka 1998.
Mmachinga alifunga mabao 26 na hadi leo ikiwa ni zaidi ya miaka 25 haijavunjwa, licha ya Abdallah Juma kuikaribia mwaka 2006 alipofunga mabao 25 huku Meddie Kagere akiwa nyota wa kigeni aliyeikaribia zaidi kwa kufunga mabao 23 msimu wa 2018-2019.
Sowah aliyefunga mabao 13 katika mechi 14 za Ligi Kuu Bara msimu uliopita akiwa na Singida BS, aliliambia Mwanaspoti kuwa, anaamini kwa ubora wa wachezaji waliopo Simba na njaa ya mafanikio waliyonayo yupo katika nafasi nzuri zaidi ya kufanya makubwa na kuisaidia timu kufikia malengo.
“Nikiwa na Singida nilifanya vizuri, lakini nilihisi bado kuna nafasi ya kufanya makubwa zaidi. Simba ni klabu yenye wachezaji wakubwa na mashabiki wanaoipa nguvu timu. Huu ni wakati wa kufanya zaidi,” alisema.
Tangu enzi za Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, rekodi ya mabao 26 ndani ya msimu mmoja imeendelea kudumu kwa miaka mingi bila kuvunjwa. Wadau wengi walitarajia kwamba kwa uwepo wa washambuliaji wengi wa kigeni ambao wamepita, rekodi hiyo ingevunjwa, lakini kwa karibu miongo mitatu sasa imeendelea kusalia. Sowah alisema hii ni changamoto anayoiweka mbele yake.
“Unapokuwa mshambuliaji, lazima ujiwekee malengo makubwa. Rekodi ipo pale siyo kwa kupendelewa, bali kwa jitihada zilizowekwa na aliyeiweka. Kwa mimi, naiona kama changamoto ambayo naweza kuikimbiza. Nataka kuipa Simba sababu nyingine ya kujivunia na mashabiki sababu ya kushangilia,” alisema.
Mmachinga, aliyewahi kuzichezea timu kama Bandari Mtwara, Simba, Mmbanga FC na Twiga Sports, alifunga mabao 26 akiwa Yanga msimu wa 1998, mbali na rekodi ya kufunga mabao mengi ndani ya msimu mmoja, straika huyo wa zamani, pia alishikilia rekodi ya kuwa mfungaji wa muda wote katika Ligi ya Bara akiwa na mabao 153 kupitia misimu 13 kuanzia 1993-2005 kabla ya kuvunjwa na John Bocco aliyefunga mabao 156 ndani ya misimu 17 kati ya 2008-2025.