Tchakei: Kwa huyu, Chama mtakoma!

KIUNGO mshambuliaji wa Singida Black Stars, Marouf Tchakei amesema usajili wa Clatous Chama ndani ya timu hiyo umeongeza ubora hasa safu ya ushambuliaji, huku akiweka wazi kuwa washambuliaji wa timu hiyo washindwe wenyewe.

Tchakei anayeitumikia Ligi Kuu kwa msimu wa tatu baada ya kutua akitokea AS Vita ya DR Congo amekuwa na mwendelezo mzuri ndani ya timu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Tchakei alisema timu hiyo msimu huu imeongeza idadi kubwa ya wachezaji bora ambao tayari wana uzoefu, huku akimtaja Chama kuwa ni miongoni mwa nyota bora na amekuwa akimfuatilia.

“Chama ni mzuri akiwa na mpira ana jicho la kutoa pasi kwa usahihi, lakini ni mzuri zaidi akiwa ndani ya 18 ana uwezo wa kufunga na kutoa pasi sahihi ambayo itazaa bao kulingana na umakini wa mchezaji aliyepewa,” alisema Tchakei na kuongeza;

“Matarajio ni makubwa naamini siku tukipana nafasi ya kucheza pamoja tutafanya kitu kikubwa kwenye safu ya ushambuliaji mimi naweza kutokea pembeni na yeye akacheza namba 10.”

Tchakei akizungumzia msimu huu katika Ligi na michuano ya kimataifa baada ya kutwaa taji la Kagame Cup 2025 alisema timu yao itakuwa na msimu bora kutokana na ubora wa kikosi walichonacho.

“Tumeanza na taji la Kagame ni mwanzo mzuri, lakini mafanikio hayo hayatufanyi tukaamini kuwa kila kitu kitakuwa rahisi, tunaendelea kujiweka imara zaidi ili kuweza kufikia malengo,” alisema Tchakei aliyefunga jumla ya mabao 15 kupitia misimu miwili.

“Kagame ni michuano ya muda mfupi kuna ligi ambayo tunakutana na zaidi ya mechi 20, mipango sahihi inatakiwa ili tuweze kufikia mafanikio.”