SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeufungia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi uliopo Tabora kutumika kwa michezo ya Ligi Kuu Bara kutokana na kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.
Taarifa iliyotolewa na TFF leo Septemba 20, 2025, imeeleza kuwa miundombinu ya uwanja huo haikidhi matakwa ya Kanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu.
“Kufuatia uamuzi huo, timu zinazotumia uwanja huo kwa michezo yao ya nyumbani zitalazimika kutumia uwanja mwingine kama Kanuni inavyoelekeza mpaka uwanja wao utakapofunguliwa, baada ya kufanyiwa marekebisho na kukaguliwa na TFF.
“TFF inazikumbusha Klabu zote kuendelea kutunza na kuboresha miundombinu ya viwanja,” ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF, Cliford Mario Ndimbo.
Kufungiwa kwa uwanja huo kumetokea saa chache baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika hapo ambapo wenyeji TRA United zamani Tabora United ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Dodoma Jiji.