Trump aangukia pua kesi ya kudai fidia ya Sh37 trilioni gazeti la The New York Times

Washington. Jaji wa Mahakama ya Shirikisho ya Florida ametupilia mbali kesi ya madai ya kashfa ya Sh37 trilioni (Dola bilioni 15 za Marekani) iliyofunguliwa na Rais Donald Trump dhidi ya gazeti la The New York Times.

Jaji Steven Merryday, aliyesikiliza kesi hiyo iliyofunguliwa Septemba 15, 2025, ametoa uamuzi huo Ijumaa, Septemba 19, 2025, na kuikosoa kwa misingi ya kiuandishi na kisheria.

Jaji Merryday kwenye hukumu yake amesema kuwa malalamiko hayo yanayohusu kitabu na makala moja yaliyoandikwa na waandishi wa The New York Times, Russ Buettner na Susanne Craig, hayakuwa sahihi kisheria.

Katika uamuzi wake wa kurasa nne, Jaji Merryday ameandika: “Malalamiko yanapaswa kuwa taarifa fupi, ya moja kwa moja, yenye kueleza madai kwa uwazi na kwa heshima ili kuwafahamisha walalamikiwa kuhusu asili na maudhui ya mashtaka dhidi yao.”

Ameendelea: “Malalamiko si kipaza sauti cha matangazo ya kisiasa, wala si jukwaa la hotuba ya jazba ya mkutano wa hadhara.

Jaji huyo amempa Trump siku 28 kuwasilisha malalamiko yaliyorekebishwa yasiyozidi kurasa 40.

Jaji Merryday amesema kesi hiyo haikuanza kuzungumzia madai halisi ya kashfa hadi ukurasa wa 80. Ameelezea kuwa malalamiko hayo yalikuwa yamejaa sifa za kupindukia kwa Trump, marudio ya hoja na lugha ya kushambulia ambayo haina nafasi kwenye hati ya kisheria.

“Malalamiko si jukwaa la umma la matusi na kejeli, wala si uwanja unaolindwa kwa hasira dhidi ya mpinzani,” ameandika Jaji Merryday, ambaye ni mteule wa Rais wa zamani wa Republican, George H.W. Bush.

Katika taarifa iliyotolewa kupitia X (zamani Twitter), msemaji wa The New York Timesaalisema gazeti hilo limepokea uamuzi wa jaji ambao umetambua kuwa malalamiko hayo yalikuwa nyaraka za kisiasa badala ya hoja za kisheria zenye uzito.

Trump alifungua kesi hiyo dhidi ya gazeti la The New York Times Septemba 15, 2025, ikiwa na malalamiko ya kukashifiwa kwenye kurasa 85 huku akidai alipwe fidia ya Dola bilioni 15 za Marekani (sawa na Sh37 trilioni).

Trump (79), amekuwa na uhasama wa muda mrefu dhidi ya vyombo vya habari, na tangu kurejea kwenye harakati za siasa, amezidisha mashambulizi hayo kwa kuwakosoa waandishi wanaomkosoa, kupunguza upatikanaji wa habari na kufungua kesi zinazodai fidia kubwa.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa mahakamani Florida, Trump alilituhumu gazeti la The New York Times kwa tabia ya kumchafua kwa nia ya chuki ya dhati (actual malice) kwa muda wa miongo mingi.

Trump alidai kuwa waandishi hao wawili “walieneza kwa makusudi simulizi isiyo na msingi” kwamba mtayarishaji wa televisheni Mark Burnett ndiye aliyemfanya kuwa mtu maarufu.

Alisema walifanya hivyo wakati ambapo walijua wazi kuwa Trump tayari alikuwa mtu mashuhuri na mfanyabiashara aliyefanikiwa, na makala ilishambulia kuhusu biashara za awali za Trump na uhusiano wake na baba yake, Fred Trump.

Pia, ilitaja makala iliyoandikwa na Peter Baker iliyochapishwa Oktoba 20, 2024, yenye kichwa: “Kwa Trump, maisha ya kashfa yakaribia hukumu.”

Ingawa Katiba ya Marekani inalinda uhuru wa vyombo vya habari, Trump amepata mafanikio katika kesi nyingine dhidi ya mashirika ya habari, akishinda fidia ya mamilioni ya dola kutoka ABC News na CBS inayomilikiwa na Paramount. Fedha hizo zinaripotiwa kuelekezwa kwenye maktaba yake ya rais atakayejenga.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.