UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI NI FURSA MPYA YA VIJANA KUINUKA

Na Pamela Mollel, Arusha.

Vijana nchini wametakiwa kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika ufugaji wa kuku wa kienyeji, kwa kuwa ni biashara yenye faida kubwa na soko pana linalokua kila siku.

Akizungumza na vijana waliomtembelea katika soko la Morombo jijini Arusha, mjasiriamali maarufu wa kuku, Mudy Musa, alisema ufugaji wa kuku wa kienyeji ni miongoni mwa sekta rahisi kuanza na inaweza kumuwezesha kijana kupata kipato cha haraka endapo atajituma na kuwa na maarifa sahihi.

“Ufugaji wa kuku wa kienyeji unaweza kukupa faida ya haraka kwa sababu nyama na mayai yake hupendwa zaidi na wateja. Ni rahisi kulinganisha na aina nyingine za ufugaji, na soko lake halina kikomo,” alisema Musa.

Aliongeza kuwa mbali na kuuza mayai na nyama, mfugaji anaweza pia kufanya biashara ya kununua kuku kutoka vijijini na kupeleka mjini, jambo linaloweza kumpatia faida kubwa zaidi.

Mudy aliwataka vijana kuiona fursa hii kama njia ya kuondokana na changamoto ya ajira na kujijengea maisha bora kupitia juhudi zao wenyewe.

Vijana waliokutana naye walionesha kufurahishwa na elimu waliyoipata moja kwa moja kutoka kwa mjasiriamali huyo, na walisema wamepata hamasa ya kuanzisha miradi ya ufugaji wa kuku wa kienyeji.

“Tumejifunza mengi. Ufugaji huu siyo tu chanzo cha kipato, bali pia unatoa uhakika wa chakula bora kwa jamii,” alisema mmoja wa vijana hao kwa furaha.