Zitto aahidi kupigania meli mpya, maisha mapya Kigoma

Kigoma. Mgombea ubunge wa Kigoma Mjini kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema kuwa iwapo wananchi wa mji huo watamrudisha tena bungeni, atahakikisha mradi mkubwa wa ujenzi wa meli na chelezo wenye thamani ya zaidi ya Sh600 bilioni unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili.

Akihutubia maelfu ya wananchi leo, Jumamosi, Septemba 20, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Bangwe, Zitto amesema mradi huo ni wa kimkakati na unaleta fursa kubwa kwa maendeleo ya Mkoa wa Kigoma na taifa kwa ujumla.

“Mradi huu ukikamilika utabadili kabisa sura ya Kigoma. Ni kichocheo cha ajira, biashara na mzunguko wa fedha. Nataka kuona ukikamilika kwa viwango na kwa wakati,” amesema Zitto.

Zitto ameongeza kuwa, wakati ujenzi wa mradi huo utakapoanza rasmi, zaidi ya watu 1,000 watapata ajira kila siku, hatua itakayochochea uchumi wa eneo hilo, hususan Kata ya Bangwe, kutokana na ongezeko la shughuli za kiuchumi.

“Huu si mradi wa Kigoma pekee, ni mradi wa kimkakati kwa Ziwa Tanganyika na nchi jirani. Tunahitaji usimamizi makini, si maneno.

“Kata yenu ina mradi mkubwa wa kujenga eneo la kujenga meli na chelezo. Mradi huu ni fursa kubwa kwa mji wetu kwani ni kichocheo cha maendeleo ya miji na wananchi watanufaika na fursa za ajira,” amesema Zitto.

Zitto pia ameahidi akichaguliwa atahakikisha anamaliza changamoto ya ukosefu wa soko katika kata hiyo, eneo lenye mzunguko wa biashara, ambapo kwa sasa kina mama wamekuwa wakipata shida sehemu ya kufanyia biashara zao.

“Eneo la Katonga, ambapo kina mama wanaweka biashara zao, hakuna soko. Wanapigwa na jua, wakifukuzwa kila wakati na mgambo, lakini hawana pa kwenda kwa sababu hakuna soko. Hivyo, mkinichagua nitasimamia ujenzi huo na wananchi wawe na soko kubwa na bora la jioni,” amesema Zitto.

Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Ngome ya Kijana wa ACT-Wazalendo, Abdul Nondo, amesema uchaguzi huo una maana kubwa kwao na ni uchaguzi utakaoheshimisha mkoa huo kwa kurejesha heshima yake iliyokuwepo awali.

“Zitto ndiye alianza kupambania miradi mbalimbali akiwa mbunge. Moja ya miradi hiyo ni ujenzi wa reli ya kisasa (SGR). Akiwa bungeni amepambania na hatimaye ujenzi huo umefika Mkoa wa Kigoma. Hivyo, tumpe nafasi akamilishe miradi mingine ambayo aliianza,” amesema Nondo.

Naye mgombea udiwani wa Bangwe, Abdallah Mandanda, amesema akichaguliwa ataanzisha miradi wezeshi katika kata hiyo kwa ajili ya kukuza uchumi wao.

“Tutajenga chuo cha ufundi katika kata yetu. Watajenga mradi mkubwa wa intaneti ambao utakuwa unazalisha vocha. Lengo ni kuboresha mawasiliano katika eneo hilo na mkoa kwa ujumla,” amesema Mandanda.