Njombe – Askari wa Gereza la Njombe, Erasto Mlelwa (26) mwenye namba C.916 WDR, amefariki dunia baada ya kujirusha kutoka kwenye gari la Polisi wakati likiwa linaenda kwa mwendo, kufuatia kuoneshwa mwili wa askari mwenzake ambaye anadaiwa kumuua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, ACP Mahamoud Banga, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa Mlelwa alijirusha akiwa ndani ya gari la Polisi lililokuwa likielekea Hospitali ya Lilondo, Madaba mkoani Ruvuma.
“Mtuhumiwa baada ya kuona mambo yako wazi aliamua kujitoa uhai wake kwa kuruka kutoka kwenye gari na kuangukia kichwa. Alipofikishwa hospitalini tayari alikuwa amepoteza maisha,” alisema RPC Banga.
Tukio hilo limeibuka kufuatia uchunguzi wa kupotea kwa askari mwingine wa Gereza la Njombe, Dickraka Mwamakula (24) mwenye namba C.681 WDR, aliyeripotiwa kutoweka Septemba 7, 2025. Kwa mara ya mwisho, Mwamakula alionekana akiwa na Mlelwa katika eneo la Lilondo kwa ajili ya kuangalia mashamba.
Baada ya upelelezi, Polisi walifika shambani walikopelekwa na watuhumiwa na kukuta mwili wa Mwamakula ukiwa umezikwa, ukiwa na jeraha kichwani na dalili za kuchomwa moto.
RPC Banga amesema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kikazi, ambapo marehemu Mlelwa alidaiwa kutoridhishwa na mwenzake kupendwa kutokana na utendaji bora wa kazi zake.
Related