Busungu wa Ada Tadea aahidi kujenga mji wa teknolojia akipewa ridhaa ya urais

Moshi. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Ada Tadea, Georges Busungu ameahidi endapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi, atajenga mji maalumu wa teknolojia utakaojumuisha wabunifu na vijana wenye ujuzi kwa ajili ya kufanya kazi za ubunifu kwa manufaa ya taifa.

Akizungumza leo Jumapili, Septemba 21, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Manyema Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro, Busungu amewaomba wananchi wamchague ili kuleta mageuzi makubwa ya kimaendeleo.

“Tupeni nafasi Ada Tadea na moja ya vipaumbele vyetu ni kurekebisha masuala ya teknolojia kwa kujenga mji maalumu wa kitaalamu wa teknolojia utakaokusanya wabunifu na vijana wenye ujuzi, kufanya kazi za ubunifu kwa manufaa ya taifa,” amesema.

Mbali na teknolojia, Busungu ameahidi kuboresha kilimo cha kahawa na mazao mengine kwa kuhakikisha yanapata masoko ya uhakika.

Amesema hatua hiyo itaongeza kipato cha wakulima huku akisema serikali ya Ada Tadea itasimamia kodi kwa haki, akibainisha kuwa wafanyabiashara wadogo hawatatozwa kodi kabla ya kupata faida.

“Kodi italipwa baada ya kupata. Mtu ambaye hajapata hatatozwa. Tunataka kujenga misingi ya watu kuwa matajiri,” amesisitiza.

Vipaumbele vingine alivyovitaja ni kuboresha usafi wa mazingira na miundombinu ya masoko ili wafanyabiashara wafanye shughuli zao katika mazingira bora.

Aidha, ameahidi kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuviwezesha vifaa vya kisasa, ikiwemo helikopta maalumu ya polisi kwa ajili ya doria na kufika haraka kwenye maeneo ya matukio.

Busungu amema serikali yake itatoa elimu bure kuanzia shule ya awali hadi chuo kikuu, pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na utawala wa uwajibikaji bila kujali chama wala itikadi.

Kwa upande wake, mgombea mwenza wa Ada Tadea, Ally Makame Issa ameahidi kushughulikia masuala ya mazingira hususan eneo linalozunguka Mlima Kilimanjaro ili kuulinda mlima huo ambao ni kivutio kikubwa cha utalii nchini.

“Tupeni nafasi Ada Tadea, tutaboresha miundombinu ya barabara na mifereji hasa maeneo ya Moshi pamoja na kutoa ruzuku kwa wakulima wanaoishi pembezoni mwa Mlima Kilimanjaro ili kulinda mazingira ya mlima huo,” amesema.

Aidha, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura Oktoba 29, 2025 na kusisitiza umuhimu wa kulinda amani ya taifa.

“Ni wakati wa kufanya uamuzi sahihi. Twende tukapige kura kwa amani kwani amani ya nchi yetu ndiyo kitu bora zaidi,” amesema.

Naye Katibu Mkuu wa Ada Tadea, Salehe Msumari amesema chama hicho kimejipanga kufufua viwanda vilivyokufa hususan mkoani Kilimanjaro, ambavyo kwa sasa vimegeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhi bidhaa kutoka nje, hali inayodidimiza uchumi wa Moshi.