Mpimbwe. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimeahidi kushughulikia tofauti za mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma endapo kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu.
Pia, kutakuwa na sera ya kuhakikisha watumishi wote wa umma wanalipwa kima cha chini cha mshahara kwa mwezi Sh800,000 baada ya makato ili waweze kujikimu kimaisha na kufurahia ufahari wa kulitumikia Taifa lao.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika leo Jumapili, Septemba 21, 2025, katika Kata ya Majimoto, Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi, mgombea urais wa Tanzania kupitia Chaumma, Salum Mwalimu amesema Serikali atakayoiongoza itahakikisha hakuna mtumishi wa umma anayehisi kuadhibiwa kwa kupelekwa kufanya kazi maeneo ya pembezoni.
“Hakuna eneo litakalokuwa la adhabu kwa mtumishi wa umma,” amesema Mwalimu. “Kama umepelekwa Mlele, Majimoto au Kavuu, mshahara wako utazingatia mazingira magumu unayofanyia kazi, tofauti na yule wa Kinondoni, Arusha Mjini au Iringa Mjini anayefanya kazi katika ofisi yenye kiyoyozi,” amesema Mwalimu.
Pia, amesema lengo ni kuhakikisha watumishi wa umma wanatendewa haki na kupewa motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi popote walipo nchini.
Amesema haiwezekani mtumishi wa kijijini apokee mshahara sawa na wa mjini ilhali hali ya maisha na mazingira ya kazi ni tofauti kabisa.

“Katika utawala wangu, hakuna mtumishi wa umma atakayepelekwa kijijini kama adhabu. Badala yake, ataenda kwa bashasha na mshahara wake utalipwa kwa kuzingatia ugumu wa mazingira,” amesema.
Mwalimu amewataka watumishi wa umma na wananchi kwa jumla kuwa na matumaini, akiahidi kuwa iwapo Chaumma itashinda, changamoto nyingi za maeneo ya vijijini zitapatiwa suluhisho la kudumu.
Katika hatua nyingine, Iddi Mabembenya mgombea ubunge wa Kavuu, kupitia Chaumma amesema wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na changamoto kubwa katika miundombinu ya barabara, upungufu wa maeneo ya malisho kwa mifugo pamoja na ukosefu wa soko la uhakika kwa mazao yao, hususan mpunga na mahindi.
Mabembenya amesema hali hiyo inarudisha nyuma juhudi za wakulima na wafugaji katika kukuza uchumi wa jimbo hilo.
“Barabara nyingi hazipitiki nyakati za mvua, hali inayosababisha wakulima kushindwa kusafirisha mazao yao sokoni kwa wakati,” amesema Mabembenya.
Pia, amesema wananchi wengi wa Kavuu wamekuwa wakilalamikia hali ngumu ya kiuchumi, huku wakihitaji msaada wa haraka kutoka kwa viongozi wao katika kuboresha mazingira ya uzalishaji na masoko ya bidhaa, hali iliyomsukuma kuomba ridhaa akawawakilishe kwenye chombo cha uamuzi.
Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chaumma, John Mrema amewataka wananchi wa Kavuu kuwa makini na viongozi wanaowachagua, akisisitiza umuhimu wa kupeleka wawakilishi wenye dira ya kweli ya maendeleo.

“Mnakabiliwa na ushuru unaotozwa kwenye mazao, kila mahali ni mateso. Mchagueni Mwalimu mwenye maono yanayothamini maisha ya Mtanzania. Acheni kuwachagua wanaokwenda bungeni kupiga makofi badala ya kuwasemea,” amesema Mrema.
Baada ya mkutano huo, Mwalimu anajiandaa kwa mkutano mwingine mkubwa wa hadhara utakaofanyika Mpanda Mjini mkoani Katavi.