Dah! Siku 765 kinyonge | Mwanaspoti

KAMA ulikuwa hujui ni Septemba 16, 2025 siku ilipopigwa mechi ya Dabi ya Kariakoo, ilikuwa ni siku 765 kamili tangu Simba ilipoonja ushindi wa mwisho mbele ya Yanga.

Ndiyo, Simba iliitambia Yanga mara ya mwisho Agosti 13, 2023 katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuzindua msimu wa mashindano wa 2023-2024 iliyopigwa Mkwakwani Tanga kwa ushindi wa penalti 3-1 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.

Baada ya matokeo hayo ya Mkwakwani, Simba imekutana na Yanga katika mechi sita za michuano tofauti na zote imechapika ikiwamo hiyo ya Ngao ya Jamii ya msimu huu iliyopigwa wiki iliyopita.

Mara baada ya kupoteza Mkwakwani kwa penalti, Yanga ilifunga mkwiji na kuikomalia Simba kwa kuifumua mabao 5-1 katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huo wa 2023-2024 kabla ya kurudia tena Aprili 20, 2024.

Kumbuka vipigo hivyo vyote vilipita mikononi kwa makocha wawili tofauti, zile 5-1 alipewa Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na kusababisha kufutwa kazi na kuletwa Abdelhak Benchikha aliyekubali kichapo cha 2-1 na kutimka klabuni kwa maelezo ana matatizo ya kifamilia.

Baada ya Benchikha kutimka aliletwa Fadlu Davids ambaye ameshuhudia vipigo vinne mfululizo  kutoka kwa Yanga na kuifanya Simba kutimiza jumla ya siku 765 ambazo ni sawa ma miaka miwili na mwezi mmoja na siku tatu au miezi 25 na siku tatu ambazo ni sawa na wiki 109 na siku mbili.

Katika Ligi Kuu Simba imepata ushindi mbele ya Yanga mara ya mwisho Aprili 16, 2023 katika mechi ya kufungia msimu wa 2022-2023 na baada ya hapo imekuwa ikinyooshwa kila inapokutana na watani wao hao wa jadi, jambo ambalo limewakata stimu Wana Msimbazi.

Kwa wanaokumbuka katika mechi hiyo mabao ya Simba yaliwekwa kimiani na beki Henock Inonga na Kibu Denis, ndipo timu hizo zikaenda kuvaaa katika Ngao ya Jamii, Yanga ikiwa chini ya Miguel Gamondi aliyepoteza kwa penalti 3-1 na kujiweka sawa kumdhalilisha Robertinho.

Robertinho licha ya kushinda mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya kufungia msimu kisha kupata Ngao ya Jamii, taji pekee ililolipata Simba kwa misimu minne mfululizo katika mashindano ya Bara, ukiacha Kombe la Muungano ililitwaa 2024 visiwani Zanzibar, alikula mkono na kufutwa kazi.

Gamondi aliendelea kugawa maumivu kwa makocha wa Simba baada ya kumdhalilisha Benchikha kwa mabao 2-1 na kumlamba Fadlu kwa bao 1-0 katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii msimu uliopita kabla ya kumfunga tena katika Ligi Kuu Oktoba 19 mwaka jana iliyokuwa ya mwisho kwa kocha huyo raia wa Argentina kukutana na Simba akiwa Yanga.

Kocha huyo alitimuliwa mwezi mmoja baadae kutokana na vipigo viwili mfululizo kutoka kwa Azam (1-0) na Tabora United (sasa TRA United) iliyowanyoa mabao 3-1, lakini kuondoka kwake hakukumsaidia Fadlu wala Simba kwani bado iliendelea kunyanyaswa.

Katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu msimu uliopita, Fadlu na Simba yake ilikumbana na kipigo cha mabao 2-0 na kuipa Yanga ubingwa ikiwa na kocha mwingine, Miloud Hamdi ambaye aliwapa pia wababe hao wa Jangwani Kombe la Shirikisho (FA) kwa kuilaza Singida BS kwa mabao 2-0.

Hamdi baada ya mechi hizo za mbili za kufungia msimu alitimkia Misri na kuletwa Romain Folz ambaye Septemba 16 katika Ngao ya Jamii aliendelea kutonesha ‘mshono’ kwa Simba kwa kuiongoza Yanga kushinda 1-0 kwa bao la Pacome Zouzoua kuhitimisha kipigo cha sita mfululizo kwa Wekundu na cha nne ikiwa chini ya Fadlu.

Katika mechi hizo sita, ukiondoa ubora wa kuchukua pointi nyingi, Yanga ndiyo timu iliyovuna mabao mengi ambayo ni 12 huku Simba ikifunga mawili tu katika vipigo vya 5-1 na 2-1 na mechi nyingine zilizobaki Wekundu hao wamekuwa wakitoka kapa kwa nyota wake kutofunga bao lolote.

Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli ndio wanaoongoza kwa kufunga mabao mengi katika mechi hizo sita mfululizo, kila mmoja akiwa na matatu wakifuatiwa na Stephane Aziz KI aliyefunga mawili.

Nyota wengine waliofunga katika mechi hizo za Dabi ya Kariakoo zilizopita ni Clement Mzize, Joseph Guede na Kennedy Musonda kila mmoja amefunga moja sawa na Fred Michael Koublan na Kibu Denis wa Simba, huku beki Kelvin Kijili akijifunga kuiongezea Yanga idadi ya mabao.