Dakika 90 zilivyoipa Yanga rekodi mpya Angola

YANGA imeanza kwa kishindo msimu mpya wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikiichapa Wiliete ya Angola kwa mabao 3-0, ikiwa kama imetanguliza mguu mmoja kufuzu hatua inayofuata ya mchujo.

Yanga imewahi kuzing’oa timu mbalimbali za Angola, lakini ushindi huo uliopatikana kwenye Uwanja wa Novemba 11, Luanda unavunja unyonge wa mabingwa hao wa Tanzania kushinda ndani ya ardhi ya Angola.

Ipo hivi, hii ni mara ya kwanza Yanga kushinda ikiwa nchini Angola baada ya mara mbili zilizopita kupoteza, lakini pia ni mara ya kwanza kwa kikosi hicho kufunga bao nchini Angola dhidi ya wapinzani wake katika mashindano ya CAF.

Hata hivyo, Yanga imekuwa na rekodi nzuri ya kuziondosha timu za Angola ilipokutana nazo katika mashindano ya CAF.

Rekodi zinaonyesha mwaka 2007 Yanga ilicheza dhidi ya Petro De Luanda katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda kwa jumla ya mabao 3-2. Mchezo wa kwanza ugenini ilipoteza kwa mabao 2-0 na nyumbani ikashinda 3-0.

Pia mwaka 2016, Yanga ilicheza dhidi ya Sagrada Esperansa na kuitoa kwa jumla ya mabao 2-1 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika. Mechi ya kwanza nyumbani ilishinda mabao 2-0, ugenini ikapoteza kwa bao 1-0.

Kama wachezaji wake wangekuwa na utulivu mkubwa pengine ingeweza kutengeneza ushindi mkubwa zaidi ya huo, baada ya kutengeneza nafasi nyingi lakini ikazitumia tatu pekee.

Kwenye mchezo huo kinara wa kupoteza nafasi alikuwa mshambuliaji Prince Dube, ambaye alitengenezewa tano peke yake lakini akatumi moja iliyoipa timu yake bao la tatu kwenye ushindi huo.

Dube pengine presha ya kutofunga ilikuwa inamuandama alionyesha kutokuwa makini kwenye kujisahihisha kupitia nafasi ambazo alizipata kwenye mchezo huo.

Hata hivyo, licha ya Dube kupoteza nafasi, lakini alikuwa na mchango mkubwa wa kuwatawanya mabeki wa Wiliete kutokana na namna anavyokimbia kwenye nafasi tofauti uwanjani.

Yanga kwenye mechi tatu kubwa ukianzia  ya Wiki ya Mwananchi kisha ukafuata mchezo dhidi ya Simba na juzi unaonyesha kwamba ukuta umeendeleza ubora kwa kucheza na nidhamu kubwa.

Yanga haijaruhusu bao lolote kwenye mechi hizo, lakini kitu kizuri zaidi ni namna mabeki na kipa walivyoiweka timu salama mbele ya wapinzani wao hao.

Kikosi cha juzi cha Yanga kilikuwa na tofauti kubwa hakuwepo nahodha msaidizi beki Dickson Job ambaye ni majeruhi, kiungo Maxi Nzengeli alianzia benchi kisha Mamadou Doumbia akianza, mshambuliaji Clement Mzize naye alianza akimweka nje Mudathir Yahya ambaye hakucheza kabisa.

Mabadiliko hayo hayakuonyesha unyonge kwa Yanga bado ikawa na kikosi kizito mbele ya wapinzani wao na kutengeneza ushindi muhimu utakaowapunguzia mzigo kuelekea mchezo wa marudiano.

Kocha wa Yanga Romain Folz ana akili kubwa ameangalia ratiba ngumu ya mechi za karibu, ametoka kucheza dhidi ya Simba mechi ngumu akashinda, usiku huohuo timu hiyo ikawafuata Wiliete, ikapata siku moja pekee ya mazoezi ya mwisho kisha ikacheza juzi.

Kama haitoshi Jumatano Septemba 24 Yanga, itakuwa uwanjani kucheza mechi yake ya kwanza ya Ligi dhidi ya Pamba Jiji na siku tatu mbele itatakiwa kuwa tena uwanjani kumalizana na Wiliete Septemba 27.

Ratiba hiyo ngumu imempata akili kichwani Folz, ambaye ametengeneza mzunguko nzuri kwa wachezaji wake ili kulinda ubora wao na bado Yanga imebaki salama ikitengeneza ushindi mzuri.

CONTE AJIPANGE KWA ANDABWILE

Kama kuna sapraizi kubwa kwenye kikosi cha Yanga ni namna kiungo mkabaji Aziz Andambwile anavyoendelea kuishangaza nchi akimlazimisha kiungo aliyetua kwa mbwembwe nyingi Moussa Bala Conte kumsubiri kwenye benchi.

Kiwango alichoonyesha Andambwile kwenye mchezo wa Simba kilishtua na jamaa akionyesha hajabahatisha akazima tena Angola kisha akafunga bao la kibabe kwa shuti la mbali.

Andambwile chini ya Folz amekuwa staa mkubwa ghafla akiendelea kumtumia salamu Conte, kwamba licha ya kuingia kipindi cha pili ana kazi ya kufanya kuthibitisha ubora wake ili aje kuanza kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Kuna ubora mwingine ameonyesha Folz kwenye mabadiliko yake, angalia alipowapa nafasi ya Edmund John na Nzengeli na Celestin Ecua walichokuja kutengeneza mabao mawili ya mwisho

Kwenye bao la pili Ecua alifanya kazi nzuri ya kuwalazimisha Wiliete kuachia mpira na ulivyonaswa akapewa Edmund kisha akaweka msumari wa pili ikiwa ni bao lake la kwanza Kimataifa.

Maxi akatoa asisti nzuri ambayo ilitengeneza bao hilo kisha baadaye kocha huyo Mfaransa, akawaingiza Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Conte ambao walikuja kuulinda ushindi huo muhimu.

Yanga ishukuru mgogoro wa mshambuliaji Joao Manha ‘Kaporal’ na klabu yake uliomfanya staa huyo kukosa mchezo wa juzi akimlazimisha kuondoka klabuni hapo.

Kaporal ambaye alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Angola, lakini pia MVP aliukosa mchezo huo kutokana na mgogoro wake na mabosi wa klabu yake, tatizo ambalo liliifanya timu yake kukosa nguvu kubwa kwenye safu yake ya ushambuliaji.