Dkt. Samia Ahimiza Amani Kuelekea Uchaguzi Mkuu – Global Publishers


Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Kisiwani Pemba, katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu za CCM, katika Viwanja vya Gombani ya Kale, Wilaya ya Chake Chake mkoa wa Kusini Pemba, Zanzibar tarehe 20 Septemba, 2025.

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi kudumisha amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu, akisisitiza kuwa hakutakuwa na vurugu wakati wa upigaji kura Oktoba 29, 2025.

Akizungumza na wakazi wa Chake Chake, Pemba Septemba 20, 2025, Dkt. Samia amesisitiza umuhimu wa wananchi kutochokozeka na kulinda mshikamano wa kitaifa.

“Nataka niwaambie kwamba katika kipindi cha miaka hii mitano tumejitahidi kusimamia utulivu wa kisiasa, usalama na amani ndani ya nchi yetu. Msichokozeke, kuweni kama mimi mama yenu, dada yenu, nachokozwa sana lakini sichokozeki. Tusiivunje amani kwa sababu ya uchaguzi,” amesema Dkt. Samia.

Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vyema kuilinda nchi wakati wote wa uchaguzi na wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kupiga kura bila hofu.

“Niwatoe hofu kwamba tarehe ya kupiga kura hakutakuwa na vurugu yoyote. Tokeni kwa wingi kapigeni kura, vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vyema kuilinda nchi hii,” amesema.