Dar es Salaam. Siku chache baada ya Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Robert Makaramba kukosoa kitendo cha askari wa Jeshi la Polisi kumshambulia wakili Deogratius Mahinyila katika Mahakama Kuu ya Tanzania, mawakili wameeleza kwamba kitendo hicho ni kuingilia uhuru wa Mahakama.
Katika tukio hilo la Septemba 15, 2025 wakati kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ikisikilizwa, Mahinyila ambaye ni pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) alikuwa akishambuliwa na askari walikuwa wakimkamata.
Kitendo hicho kimeibua hisia tofauti kutoka kwa wadau mbalimbali wa haki ambao wamesema ni kuingilia uhuru wa Mahakama kwani polisi hawakupaswa kueleza kwamba Mahakama imejaa na isingeweza kupokea watu zaidi, bali uongozi wa Mahakama ndiyo ulitakiwa kufanya hivyo.
Alichokisema Jaji Makaramba
Akizungumzia tukio hilo kwenye majadiliano ya Jukwaa la mawakili vijana, Jaji mstaafu, Makaramba amehoji endapo wakili akishambuliwa na askari eneo la Mahakama, wajibu wa Mahakama ni upi ili kuzuia kutotokea kwa jambo hilo.
“Nilikuwa naangalia hiyo video kupitia mtandao, ilikuwa si tukio la kiutu, ni kudhalilisha, sasa nadhani polisi wetu sijui nini kimetokea, kuna mikataba ya kimataifa inayowalinda wanasheria kwenye kazi zao ikijumuisha na maeneo yao ya kufanyia kazi.
“Zipo namna hata za kumkamata wakili, tukiendelea namna hiyo inaonekana basi ni rahisi kuwapiga majaji wakiwa mahakamani, ndiyo maana yake, unaingia tu unavamia,” amesema Jaji Makaramba.
Jaji Makaramba amesema sheria ya sasa inaeleza vizuri kuhusu eneo la Mahakama, nani mwenye mamlaka ya kusimamia eneo hilo, polisi watatoa ulinzi kama wameitwa ikiwa itaonekana ni lazima kufanya hivyo.
Jaji huyo amesema japo hajui nani aliyeanzisha fujo hizo, lakini kazi ya polisi ni kulinda usalama na sio kuanzisha fujo. Alisema alishangaa video hiyo ikionyesha kijana aliyevaa fulana akivamiwa na askari watano, akisisitiza kwamba askari wawili wangetosha kumkamata, sio kundi lile.
“Kwa maoni yangu waliitia najisi Mahakama, hadi nikapata mawazo, sasa Mahakama ipate jeshi lake la kuilinda, maana yake kama Jeshi la Polisi haliwezi kulinda Mahakama na maofisa wa Mahakama,” amesema jaji huyo mstaafu.
Mawakili wakubaliana naye
Akizungumzia kauli ya Jaji Makaramba, Wakili Edson Kilatu amesema anaunga mkono kauli aliyoitoa jaji huyo kwani mahakama kulingana na Ibara ya 4 ya Katiba ya Tanzania ni muhimili unaojitegemea.
“Kwa kuwa Mahakama ni muhimili unaojitegemea, utaratibu wa kuendesha mambo yake hauwezi kupangwa na mhimili mwingine, polisi ni sehemu ya mhimili wa Serikali, kwa hiyo hatutegemei mhimili mwingine kwenda kutoa utaratibu wa namna ya kuendesha mambo mahakamani, kufanya hivyo ni kama mhimili huo umeanza kuingiliwa,” amesema.
Wakili Kilatu amesema suala la ulinzi polisi wanapofika mahakamani ni lazima wazingatie utaratibu uliowekwa na Mahakama na sio kwenda kujiamulia kile wanachotaka wao.
Amesema kama ukumbi wa Mahakama umejaa, chombo hicho ndicho cha utoaji haki nchini, ndicho kitatoa maelekezo na endapo ni suala la kelele, pia, mamlaka ya kuwanyamazisha wanaofanya hivyo itabaki chini ya mahakama na sio mhimili mwingine.
Mtaalamu huyo wa sheria ametolea mfano bungeni akisema hakuna polisi wanaokwenda kuzuia watu kule kutokana na chombo hicho kuwa na utaratibu wake akihoji inawezekanaje watu kupigwa mahakamani.
“Mtuhumiwa akiwa kizimbani hata polisi hapaswi kuwepo mbele ya kizimba ameficha uso, hiyo inamsababisha mtuhumiwa kutishika ndio maana mtuhumiwa akifika mahakamani pingu zinafunguliwa kwa sababu mtu hana hatia hadi itakapothibitika vinginevyo,” amesema.
Wakili Michael Mwangasa ameunga mkono kauli ya jaji huyo akisisitiza kwamba kiongozi huyo ana uzoefu mkubwa kwenye masuala ya sheria na yupo huru kutetea misingi na Katiba ya Tanzania.
“Hili ni suala la kisheria, mahakama ni muhimili unaojitegemea, sasa huwezi kukuta askari wamekaa bungeni wakizuia watu kuingia bungeni kwa madai Bunge limejaa, utaratibu wote wa Bunge linafanywa na uongozi wa Bunge na siku zote ukifika mahakamani jaji ana walinzi na kuna walinzi wa Mahakama, hakujawahi kutokea vurugu yoyote iliyosababishwa na wananchi mahakamani wakati wa kusikiliza kesi,” amesema.
Wakili Mwangasa amesema kilichofanyika mahakamani ni jambo la ajabu hasa kuzuia watu kusikiliza kesi ndani ya mahakama ya wazi ambayo mtu yeyote anaruhusiwa kufika kusikiliza kesi.
Amesema polisi hawana jukumu lolote la kisheria ambalo wamekabidhiwa kufanya ulinzi bila maagizo ya jaji kiongozi, msajili wa mahakama au majaji wengine waliopo mahakamani.
Kwa upande wake, Wakili Hekima Mwasipu amesema tukio la polisi kumvuta nje wakili ndani ya chumba cha Mahakama na kumpiga, ni sawa na kuinajisi chombo hicho cha utoaji wa haki nchini.
Wakili Mwasipu anajenga hoja yake akisema wakili Mahinyila alikuwa kwenye majukumu yake ya uwakili ndani ya chumba cha mahakama na kama wakili huyo alikuwa na kosa la jinai, upo utaratibu uliopaswa kufuatwa ili kumkamata.
“Wakili Mainyila alikuwa akitekeleza majukumu yake ndani ya chumba cha Mahakama na polisi kuingia ndani na kumvuta na kuanza kuvutana naye, lile sio tukio tu la kinyama bali halipaswi kuvumilika mahakamani,” amesema.
Wakati mawakili wakieleza hayo, tayari Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) limepanga kufanya maandamano ya amani nchi nzima, kulaani kitendo cha kushambuliwa kwa Wakili Mahinyila na askari polisi Septemba 15, 2025 akiwa mahakamani.
Kulingana na TLS, maandamano hayo yatashirikisha mawakili wote nchini na yataambatana na tamko litakalosomwa kwa pamoja na viongozi wa mikoa.
“TLS ipange na kutangaza siku ya maandamano ya amani kwa mawakili wote nchini, kama ishara ya kupinga unyanyasaji aliokumbana nao Wakili Mahinyila na wanasheria wengine waliowahi kudhalilishwa wakiwa kazini kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Chama hicho kimeeleza kuwa lengo kuu ni kulinda heshima, utu na usalama wa wanasheria, kikisisitiza kuwa kushambulia wakili mmoja ni kuishambulia taaluma nzima na kuathiri ustawi wa haki nchini.
Mbali na maandamano, TLS ilitangaza hatua ya kusitisha ushiriki wa mawakili katika kesi zote za msaada wa kisheria za jinai pamoja na shughuli zinazohusiana na Mahakama na Serikali, mpaka pale hatua za kisheria zitakapochukuliwa dhidi ya askari waliomshambulia Mahinyila.
“Kuanzia sasa mawakili wasikubali kupewa au kushughulikia kesi mpya za msaada wa kisheria kutoka mahakamani hadi tutakapopata taarifa rasmi kuwa hatua zimechukuliwa dhidi ya wote waliohusika. Taarifa ya kusitisha kesi hizo iwasilishwe mara moja kwa Mahakama na upande wa Jamhuri,” imeeleza taarifa hiyo.
TLS pia imepanga kufungua mashauri dhidi ya askari waliohusika katika tukio hilo, huku likiahidi kumsaidia Mahinyila katika hatua zote za kisheria.
Chama hicho kimeitaka Serikali, Mahakama na Jeshi la Polisi kutoa tamko na kuchukua hatua stahiki za kisheria ili kuwawajibisha waliohusika.
Wakati TLS wakipanga kuandamana, Septemba 15,2025, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amefafanua kwamba wakati kesi ya Lissu ikiendelea, lilijitokeza kundi la wanachama wa Chadema baada ya ukumbi uliokuwa unatumiwa kwenye kesi ya Lissu kujaa, kuanzisha fujo.
Kamanda Muliro amesema baada ya kuanzisha fujo hizo na kujaribu kuwashambulia askari walijihami na kutuliza fujo hizo haraka.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kuwa kitendo chochote cha kuwachokoza askari kitashughulikiwa haraka na kuyarejesha mazingira ya usalama kwenye eneo husika haraka kwa kadiri inavyowezekana,” amesema.
Wakati huohuo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ilemele, Egnatus Kapira, akijibu barua ya maandamano ya mawakili yaliyopangwa kufanyika wilayani humo, alisema maandamano hayo yanaingilia ratiba ya kampeni za uchaguzi.
Maandamano hayo yalipangwa kufanyika kuanzia Mtaa wa Buswelu Centre Wilaya ya Ilemela na kuhitimishwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Masjala ya Mwanza.
“Kutokana na tarehe ambayo mmeitaja kufanya maandamano inaingilia ratiba ya kampeni za uchaguzi mkuu ambazo zilizinduliwa rasmi Agosti 28, 2025 hadi Oktoba 28, 2025 kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,” imeandikwa kwenye barua hiyo.
Kulingana na barua hiyo, Kamanda Kapira ameelekeza kuwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Ilemela halitakuwa na nafasi ya kutoa ushirikiano kuhakikisha maandamano yanafanyika kwa usalama kwa kuzingatia kwamba jeshi hilo linahusika katika kusimamia kampeni za uchaguzi.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limezuia kufanyika maandamano hayo kutokana na sababu hizo.
Katika hatua nyingine, Chadema kililaani kitendo cha Jeshi la Polisi kumshambulia na kumdhalilisha Wakili Mahinyila pamoja na baadhi ya viongozi na wanachama wengine.
Kwa mujibu wa Chadema, wakili Mahinyila alishambuliwa, kujeruhiwa vibaya na kudhalilishwa na askari katika eneo la Mahakama alipokuwa akihudhuria kesi ya uhaini inayomkabili Lissu.
Chama hicho kililitaka Jeshi la Polisi kuheshimu eneo la Mahakama na Watanzania wanaofika eneo hili kufuatilia kesi mbalimbali.