Ligi ya Kriketi Wasichana nguvu yahamishiwa Dodoma

CHAMA cha Kriketi nchini (TCA)  kimeazimia kulifanya Jiji la Dodoma kuwa makao makuu ya mchezo wa kriketi na kuzidi kuhamasisha hasa wanawake kushiriki.

Mkufunzi wa Kriketi Dodoma, Benson Mwita alisema wanataka kuhakikisha mchezo huo unakuwa kati ya inayopendwa na wanawake shuleni.

“Mwitikio wa vijana ni mkubwa na wengi, hasa wasichana wametokea kuupenda mchezo huu. Naamini miaka michache ijayo kriketi itakuwa ni mchezo pendwa kwa wasichana nchini,” alisema Mwita.

Aliishukuru serikali kwa kubali kuingiza kriketi katika michezo ya shule za Sekondari (UMISSETA) na mwaka huu Dodoma umekuwa mmoja wa washindi kwa timu za Sekondari ya Kizota A na B kuibuka kidedea katika Ligi ya TCA kwa wasichana ikiwa inatafuta kinara wa mizunguko 20 (T20).

Katika mchezo wa kwanza Kizota B iliifunga Ihumwa kwa mikimbio 12.  

Kizota B ndiyo iliyopata kura ya kuanza na kupiga mikimbio 46 baada ya kupoteza wiketi zote 10 ikiwa imetumia mizunguko 15 kati ya 20.

Ingawa ni alama ndogo, lakini mikimbio 46 ilionekana ni mlima mrefu sana kwa Shule ya Sekondari ya Uhumwa baada ya kujikuta ikimaliza mizunguko yote 20 na  kuambulia mikimbio 34, hivyo kupoteza kwa mikimbio 12.

Waliochangia ushindi wa Kizota B ni Flora William aliyetengeneza mikimbio sita kutokana na mipira 22, Munira Godfrey aliyepiga mikimbio mitano kutokana na mipira 21 na Mgeni Juma mikimbio  minne kutokana na mipira     nane.

Katika mchezo mwingine, Kizota A iliifunga Kaloleni kwa jumla ya mikimbio 17.

Kizota A ndiyo iliyoanza kubeti na kufikisha mikimbio 68 baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 14 kati ya 20 ya mchezo huo.

Jitihada za Shule ya Wasichana Kaloleni kuifukuzia mikimbio 68 hazikufua dafu baada ya kujikuta wakigota kwenye mikimbio 51 baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 13 kati ya 20 ya mchezo huo na mwisho wakapoteza kwa mikimbio 17.

Mashujaa wa ushindi wa Kizota A walikuwa ni  Mariam Omary aliyecheza mikimbio 12 kutokana na mipira 24, Anna Mgalama aliyepiga mikimbio 11 kutokana na mipira 14 na Vaileth Elisante aliyeongezea mikimbio nane kutokana na mipira 13.