KIUNGO wa Shamakhi FC inayoshiriki Ligi Kuu Azerbaijan, Alphonce Mabula amesema huu unaweza kuwa msimu wake bora na wenye mafanikio tangu aanze kucheza soka la kulipwa.
Kabla ya kutimkia Shamakhi kiungo huyo aliwahi kuitumikia FK Spartak Subotica ya Ligi Kuu ya Serbia maarufu kama Serbian SuperLiga kwa misimu miwili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mabula alisema msimu huu unaweza kuwa njia ya kufika Ligi Kubwa Ulaya kama atakuwa na mwendelezo wa alichokianza kwenye mechi nne.
“Kila mchezaji ana malengo yake, natamani sana yale niliyoyapanga yatimie na nafikiri kwa kiwango nilichoanza nacho inaweza kuwa tiketi ya kwenda kucheza Ulaya,” alisema Mabula na kuongeza;
“Ligi imeanza kwa kwasi sana yaani timu ikizubaa kupata ushindi ngumu kwa sababu karibu timu zote zimesajili wachezaji wenye uzoefu kutoka Urafansa, Hispania na ligi nyingine na huko hakuna kikomo cha kusajili wachezaji wa nje.”
Kwenye mechi nne alizocheza kiungo huyo wa chini amefunga bao moja na kutoa asisti moja akisaidia chama lake lililopo nafasi ya sita kukusanya pointi tano.
Kiungo huyo wa Taifa Stars amekuwa na muendelezo wa kiwango bora tangu msimu uliopita ambao aliingia dirisha dogo na kuingia moja kwa moja kwenye kikosi akicheza mechi 17 na kufunga mabao matatu.