Matumaini mapya Mv New Mwanza ikianza safari kuelekea Bukoba

Mwanza. Matumaini mapya yameibuka katika Jiji la Mwanza baada ya meli mpya na ya kisasa nchini, Mv New Mwanza, kuanza safari yake ya nne ya majaribio kuelekea Bukoba mkoani Kagera inayotarajiwa kuthibitisha ukamilikaji wa asilimia 100 wa mradi huo wa ujenzi.

Akizungumza leo Jumapili Septemba 21, 2025 kabla meli hiyo kuanza safari ya Bukoba, katika Bandari ya Mwanza Kusini, Nahodha wa Mv New Mwanza, Bembele Mwita amesema safari hiyo ni muhimu kwa sababu ndiyo ya kwanza kufika umbali mrefu tangu meli hiyo ianze majaribio.

Ameeleza kuwa, kutoka Mwanza hadi Bukoba ni zaidi ya maili 100 za majini, hivyo wakitarajia kutumia saa sita hadi saba kulingana na hali ya hewa ndani ya ziwa na wakirudi watakuwa na majibu ya mwisho ya ubora wa mifumo na mitambo ya meli hiyo.

“Lengo la safari ya leo ni kujiridhisha uwezo wa mashine, mitambo, na mifumo ya vifaa vilivyofungwa kuweza kuhimili safari ndefu, maana kama tungechukulia tu hizi safari za kawaida, tunatembea saa tatu unarudi, hauna ule uhakika wa mifumo iliyofungwa kufanya kazi kwa ufanisi kama inavyotarajiwa au kuzungumzwa kwenye mikataba.

“Kwa hiyo baada ya safari hii ndefu na kurudi, mitambo yote itakuwa imetoa majibu kila kitu kimekaa vizuri. Tutakaporudi tutakuwa na jibu la kusema meli imekamilika hiyo asilimia moja iliyobakia itakuja kutamkwa baada ya majaribio kukamilika,” amesema Mwita.

Sababu za ujenzi kuchelewa

Meli hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2019 baada ya mkataba wake kusainiwa mwaka 2018 na mkandarasi wa Kampuni ya Gas Entec Ship-Building Engineering ya Korea kwa Sh120 bilioni, ilitakiwa kukamilika baada ya miezi 24.

Meli ya Mv New Mwanza ikianza safari kuelekea Bukoba mkoani Kagera, ikiwa ni jaribio la mwisho la masafa marefu kabla haijaanza kufanya safari rasmi. Picha na Saada Amir

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico), Eric Hamissi amesema mradi huo ulikabiliwa na changamoto nyingi na ndiyo maana ulichukua muda mrefu kukamilika.

“Mradi wetu wa ujenzi wa Mv New Mwanza umekamilika una asilimia 99, hili jaribio tunalolifanya ndio litakalokamilisha asilimia 100 lakini sasa hivi tumefika asilimia 99 ya ujenzi.

“Ninashukuru kwa kweli kwa sababu mradi ulikuwa na changamoto nyingi huko nyuma hususani kile kipindi cha ugonjwa wa Uviko-19, mradi ulisimama kwa muda mrefu lakini uliweza kurudi tena,” amesema Hamis.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni wataalamu hawakuweza kufika kwa wakati na usafirishaji wa vifaa ulikwama, bei ya vifaa muhimu ilipanda, jambo lililoongeza gharama. Pia, kulikuwa na ucheleweshaji wa uingizaji wa vifaa maalumu kutoka nje.

“Lakini kufika hatua hii, ni suala la kushukuru wataalamu wetu ambao walifanya kazi usiku na mchana, mkandarasi ambaye alijitahidi pamoja na changamoto zilizojitokeza kuhakikisha huu mradi unafika hatua hii. Watanzania tuna cha kujivunia tumejenga meli ya kwanza kubwa katika ukanda wa maziwa makuu hapa Mwanza na imejengwa na Watanzania wenyewe kwa asilimia 100,” ameeleza Hamis.

 “Leo hii tunasema tumefika asilimia 99 na safari hii ndiyo inakamilisha asilimia moja ya mwisho. Ni fahari kwamba, meli hii kubwa imejengwa na Watanzania kwa asilimia 100. Wataalamu kutoka Korea walikuwa wachache mno, chini ya 10, lakini Watanzania zaidi ya 200 ndio waliofanya kazi hii.”

Hamis ameeleza kuwa, wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, meli hiyo ilikuwa imefikia asilimia 40 ya ujenzi wake na fedha zilizokuwa zimelipwa ni Sh36 bilioni pekee, sawa na asilimia 30.

Meneja wa mradi wa meli hiyo, Vitus Mapunda amesema ujenzi wake umeacha alama kubwa kwa Taifa kwa sababu umeongeza ujuzi kwa Watanzania.

“Tumeonyesha uwezo mkubwa. Sasa tuna wataalamu wazawa waliopata uzoefu wa moja kwa moja wa kujenga meli kubwa. Taifa hili lina maziwa makuu na Pwani ndefu, hivyo tunahitaji vyombo vya kisasa. Meli hii ni hatua ya maendeleo itakayowezesha biashara na usafirishaji wa watu kwa gharama nafuu,” amesema.

Akizungumza baada ya kuikagua meli hiyo kabla ya kuanza safari kuelekea Bukoba, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema kuanza kwa safari za meli hiyo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa kanda ya Ziwa Victoria.

“Nakumbuka kipindi fulani hapa tulikuwa na ajali kubwa sana ya boti, boti imechanganya mizigo na abiria tukaenda kufanya uokozi pale watu kadhaa walifariki. Moja kati ya kilio cha wananchi ilikuwa ni kuwa na meli nzuri za kisasa ndani ya Ziwa Victoria. Kwa hiyo, wale waliokuwa wanaenda Gozba (kisiwa) sasa mkombozi ni hii meli,”amesema Mtanda.

Ameongeza kuwa, Serikali pia imewekeza katika kujenga kituo kikubwa cha uokozi na upeanaji taarifa ndani ya Ziwa Victoria kitakachokuwa na mitambo ya kisasa ya kutoa msaada wa haraka pindi ajali zinapotokea.

“Suala la usalama pia, limezingatiwa hata ikijitokeza ajali sasa hivi tutakuwa na kituo kikubwa cha uokozi hapa,”ameongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Lushinge amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho iliyoelekeza ujenzi wa miundombinu ikiwamo ya majini.

“Niwaombe wananchi wetu sasa, hii ni fursa sasa kuna biashara zitakuwa Mwanza, Kisumu, Uganda…kwa hiyo ni fursa mpya kwa meli hii baada ya ukamilishwaji wake,” amesema.

Inaelezwa, Mv New Mwanza ni meli kubwa zaidi kuwahi kujengwa nchini na ni ya kwanza kujengwa kikamilifu na Watanzania kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Korea Kusini.

Meli hiyo ina urefu wa mita 92.6, upana wa mita 17, uzito wa tani 3, 500 na ina ghorofa nne.

Ina uwezo wa kubeba abiria 1,200, mizigo yenye uzito wa tani 400 na magari 20, yakiwamo matatu makubwa.

Aidha, inatembea kwa kasi ya knoti 16, sawa na takribani kilomita 30 kwa saa, jambo linaloifanya kufika Bukoba kwa muda wa saa sita hadi saba, tofauti na meli ya sasa ya Mv Victoria inayotumia saa 10 kwa safari hiyo.

Meli ya Mv New Mwanza itakuwa na madaraja tofauti kwa ajili ya abiria kulingana na mahitaji na uwezo wao kiuchumi.

Ndani ya meli hiyo, kutakuwa na daraja la hadhi ya juu (VVIP) lenye uwezo wa kuhudumia abiria wawili, daraja la watu mashuhuri (VIP) litakalobeba abiria wanne, daraja la kwanza litakalohudumia abiria 60 na daraja la biashara llitakalobeba abiria 100.

Madaraja mengine ni la pili litakalotumiwa na abiria 200 na daraja la uchumi litakalobeba abiria 836.

Kwa kuanzia, safari zake zitakuwa zikihusisha Mwanza, Bukoba kupitia Kemondo, huku mazungumzo yakiendelea ili ianze pia kwenda nchini Uganda.