Moshi. Mgombea ubunge wa Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo maarufu Ibraline, amewaomba wananchi kumpa ridhaa ya kuwatumikia bungeni ili kuhakikisha hoja za maendeleo ya jimbo hilo zinapewa kipaumbele na si masilahi yake binafsi.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika leo Jumapili Septemba 21, 2025 katika Viwanja vya Netball Reli, Kata ya Njoro, Shayo amesema dhamira yake si kutafuta masilahi binafsi bali kutumia nafasi ya ubunge kuhamasisha maendeleo ya Moshi na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja na jimbo kwa jumla.
“Mimi sina njaa, namshukuru Mwenyezi Mungu niko vizuri. Nimeamua kugombea ubunge kwa sababu nataka kutumia nafasi yangu bungeni kuhakikisha wananchi wa Moshi wanapata mabadiliko ya kweli ya kimaendeleo,” amesema Shayo.
Katika mkutano huo, Shayo ametaja vipaumbele vyake ikiwamo kukamilisha Uwanja wa Ndege wa Moshi, hatua ambayo amesema itachochea ukuaji wa uchumi.
“Uwanja wa Ndege wa Moshi umeanza kukarabatiwa lakini bado haujakakilika, nipeni nafasi Oktoba 29, 2025 nipeleke hoja bungeni ili kupata fedha za kukamilisha uwanja wetu wa ndege. Ni wazi uwanja ule ukikamilika utachochea ukuaji wa uchumi kwa kiasi kikubwa,” amesema.
Kipaumbele kingine alichokitaja ni mikopo nafuu kwa vijana, akieleza kuwa endapo atachaguliwa ataanzisha mfuko wa mikopo yenye riba nafuu kwa waendesha bodaboda na bajaji ili kuwaondoa kwenye mikataba kandamizi na kuwapa uwezo wa kujitegemea.
“Lakini pia, nitashughulikia changamoto za barabara hasa katika maeneo ya pembezoni kuhakikisha zinajengwa kwa kiwango cha lami. Kwenye eneo lenye msongamano mkubwa kama Mbuyuni, nitapambana kuhakikisha panafungwa taa za kudhibiti magari (traffic lights)” amesema Shayo.
Shayo pia ameipongeza Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Moshi katika Kata ya Ng’ambo, akisema amesema akichaguliwa atapambana kuhakikisha fedha zinapatikana ili kukamilisha ujenzi huo.
“Rais wetu ameonesha dhamira ya dhati katika kuinua maendeleo ya wananchi wa Moshi. Tumeshuhudia miradi ya afya, elimu na hata miundombinu ya barabara. Ni wajibu wetu kumpa kura nyingi ili awe na nguvu zaidi kuendeleza kazi aliyoianza,” amesema Shayo.
Katika mkutano huo, mgombea udiwani wa Kata ya Njoro, Zuberi Kidumo amewaomba wananchi kuwaunga mkono wagombea wote wa chama hicho akiwamo Samia Suluhu Hassan, Shayo na madiwani, akisema mshikamano wao ndiyo nguzo ya mafanikio.
Kidumo, pia, ameahidi kukarabati Uwanja wa Netball Reli Njoro, kwa kupanda nyasi za kisasa na kufunga taa ili kuwawezesha kinamama na vijana kuendelea kutumia uwanja huo kwa michezo na mazoezi hata nyakati za jioni.
“Oktoba 29, 2025 tuhakikishe tunampa kura nyingi …Samia, Shayo kwa ubunge na mimi Zuberi kuwa diwani ili kwa pamoja tuendelee kuleta maendeleo ya Kata ya Njoro na mji mzima wa Moshi,” amesema Kidumo.