Moshi. Mgombea udiwani wa Kibosho Magharibi, Wilaya ya Moshi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Deo Mushi, ameahidi kuwa endapo atachaguliwa kuwa diwani, asilimia 60 ya mapato yanayokusanywa kupitia Vyama vya Ushirika wa Mazao (Amcos) yataelekezwa katika kuboresha lishe ya wanafunzi kwenye shule zote ndani ya kata hiyo.
Amesema kuwa, hatua hiyo inalenga kuboresha maendeleo ya elimu kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula bora shuleni, jambo litakalosaidia kuongeza ufaulu na mahudhurio mazuri ya wanafunzi.
Akizungumza leo Jumapili, Septemba 21 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo, amesema ndani ya kipindi cha muda mfupi atahakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa chakula shuleni kutokana na ugumu wa maisha kwa wazazi.
“Jambo linalonisumbua kuliko vyote pamoja na uchakavu wa shule zetu ni chakula cha watoto shuleni, mpango nilionao ambao nitasimama nao, ninyi mniombee mwakani wazazi msilipe mchango wa chakula shuleni,” amesema Mushi.
Amebainisha kuwa, kuanzia Januari mchango wa chakula kwa wanafunzi hautakuwepo, “mtatukuta kule shuleni, lakini ili nifanikishe hilo na ninyi nawahitaji mnipe ushirikiano kwa kunipa kura za kutosha.”
“Najua kwenye Amcos zetu kuna mamilioni ya fedha, asilimia 60 ya hizi fedha ni zenu ninyi, hizi fedha tutazipeleka kwenye chakula cha wanafunzi, hatuna ugomvi na hii fedha, tunataka hiyo asilimia 60 nipeni kura nikapiganie hili, utaratibu wa kuzipata hizi fedha nazijua,” amesema Mushi.
Mushi amesema harakati hizo zinahitaji ushirikiano wa pamoja watakaompa katika kipindi hiki ambacho ana unahitaji mkubwa wa kuwaongoza wananchi wa kata hiyo.
“Tutawaita walimu wakuu wa shule zote za kata hii watupe gharama za chakula na tukishajua gharama za mwaka mzima tutagawanya ile fedha ya ‘Amcos’ watuambie ni kiasi gani maana asilimia 60 ni yenu ninyi na asilimia 40 ni yao,” amesema Mushi.
Christina Joseph, mmoja wa wakazi wa kata hiyo, amesema endapo matarajio ya diwani huyo yatafanikiwa itakuwa ni msaada mkubwa sana kwa wananchi hasa wale ambao kipato chao ni kidogo.
“Suala la wazazi kuchangia chakula shuleni ni changamoto kwa baadhi ya wazazi kwasababu wapo wazazi ambao utafutaji wao ni wa shida na wakati mwingine wanashindwa kumudu hizo gharama,” amesema mwananchi huyo.