Mke amkata uume mumewe Manyara, wivu wa mapenzi watajwa

Hanang. Mkazi wa kitongoji cha Maweni kijiji cha Kidangu, kata ya Endagaw, wilayani Hanang mkoani Manyara, Veronica Muhale (40), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kudaiwa kumjeruhi mume wake Josephati Kasi (45) kwa kumkata kwa kisu na kuondoa sehemu zake za siri.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Maweni, Mohamed Ramadhani akizungumza na waandishi wa habari leo  Septemba 21, 2025 amesema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Septemba 19, 2025,

Ramadhani amesema chanzo cha tukio hilo ni wivu wake wa mapenzi ambao ulikuwa ni ugomvi wao wa mara kwa mara.

Inaelezwa kuwa Veronica baada ya kuukata uume wa mumewe usiku aliutupa nje ya nyumba yao.

“Ndugu zangu waandishi wa habari ni kweli uume wake ulikatwa, mimi niliukuta umetupwa hapa nje, kiungo hiki tukakiweka kwenye chombo, kisha tukarudisha ndani kwake,” amesema Ramadhani.

Mmoja kati ya wakazi wa kijiji hicho Aloyce Sanka amesema mwanamke hiyo alimvizia mume wake akiwa amelala na kumkata uume wake kwa kutumia kisu.

“Baada ya kutekeleza tukio hilo, Veronica alijisalimisha mwenyewe katika Kituo cha Polisi Katesh na kuwaeleza ndugu na jamaa wasimsake, na akibainisha kuwa yeye ndiye aliyefanya kitendo hicho cha kikatili,” amedai.

Ameendelea kudai kuwa kwa muda mrefu mwanamke huyo amekuwa akijaribu kumdhuru mume wake kwa kutumia sumu ya panya bila mafanikio.

Amedai hata kisu alichokitumia kuukata uume wa mumewe kilikuwa kimehifadhi ndani muda mrefu.

“Alimvia mumewe akiwa amelala usiku, akamfunga kwa kamba na shuka kitandani kisha akamkata sehemu zake za siri.”

“Ila inadaiwa mwanamke huyu hakutekeleza hili tukio peke yake, pia alikuwa na matatizo ya kiafya.”

‘Baada ya tukio hilo majeruhi huyo alikimbizwa mjini Babati katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kwa ajili ya matibabu,” amesema Sanka.

Emmanuel Salao, jirani wa Veronica na mumewe,  amesema mwanamke huyo amekuwa na tabia ya kumuonea wivu mume wake kila mara na amekuwa akimtishia kumuua.

Salao amesema mume wa mwanamke huyo alikuwa analalamikia kitendo cha mkewe kuwa na wivu wa kupindukia na kumtishia kumuua ili wakose wote.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo,  Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani amesema ni kweli limetokea na mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi.

“Majeruhi amepelekwa hospitali ya mkoa kwa ajili ya matibabu na mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi kwa sasa kwa mahojiano zaidi,”amesema Kamanda Makarani.