MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Oscar Evalisto anayekipiga Makadi FC ya Misri ameibuka na tuzo ya mchezaji bora wa mechi dhidi ya Maraga FC akisema zawadi hiyo ni maalumu kwa baba yake mzazi aliyefariki dunia wiki iliyopita.
Huu ni msimu wa pili kwa mshambuliaji huyo kuitumikia Makadi. Msimu uliopita alicheza miezi sita akitokea Mlandege na aliwahi kupita Paje Star ya Zanzibar na Lipuli U-20.
Akizungumza na Mwanaspoti, Evalisto alisema tuzo hiyo ni mahususi kwa baba yake aliyefariki wiki iliyopita baada ya kuugua kwa takribani miezi miwili.
“Acha tu nimehangaika na baba hospitali miezi miwili ile niliyokuwa likizo yaani nasafiri kujiunga na timu na yeye anafariki dunia, imeniuma sana na kila ninachofanya sasa hivi ni kwa ajili yake kwa sababu nisingecheza kama siyo hamasa yake,” alisema Evalisto na kuongeza’
“Tuzo hiyo tulikuwa tunawania wachezaji wawili, nilifunga mabao mawili na kipa alifanya ‘save’ moja, kwa hiyo zilipigwa kura na mimi nikachaguliwa kuwa nyota wa mchezo.”
Aliongeza pamoja na kuanza kufunga bado kikosi hicho kila mchezaji ana nafasi ya kucheza na kuanza kutokana na ushindani mkubwa kwenye eneo la ushambuliaji.
Mshambuliaji huyo alisajiliwa dirisha dogo msimu uliopita akicheza mechi nne na kufunga mabao matatu, timu hiyo ikimaliza nafasi ya sita kati ya 10 kwenye msimamo wa ligi daraja la kwanza.