NMB Yapokea Tuzo ya Uwajibikaji wa Kijamii Katika Elimu kwenye Tuzo za Mufti 2025

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema kuwa  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua kwa dhati mchango wa madhehebu ya dini ikiwemo BAKWATA na wadau wote wa elimu katika kuimarisha maadili, kuendeleza maarifa na kuleta mshikamano wa kitaifa kupitia elimu.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Mufti za Elimu 2025 zilizofanyika kwenye ukumbi wa Serena Hotel jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kusimama kidete kuhakikisha elimu inakuza maarifa na ujuzi, sambamba na malezi yanayoimarisha tabia bora na maadili ya kizalendo kwa vijana wa Kitanzania.

Katika hafla hiyo, Benki ya NMB ilitunukiwa Tuzo ya matokeo Chanya na Uwajibikaji wa Kijamii katika Elimu (Social Impact & Corporate Social Responsibility in Education Award) kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kusaidia na kuendeleza sekta ya elimu nchini. 

Tuzo hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kupokelewa kwa niaba ya benki na Mkuu wa Idara ya Masoko, Mawasiliano na Mahusiano ya Umma, Rahma Mwapachu.

Kupokea tuzo hii kumeimarisha dhamira ya NMB katika kuendelea kushirikiana na Serikali, taasisi za dini na wadau wengine kuhakikisha elimu inakuwa jumuishi, bora na endelevu, huku tukichangia malezi ya kizazi chenye maadili na maarifa kwa mustakabali wa taifa letu.