NEO Maema ni mmoja wa nyota wapya waliosajiliwa msimu huu na Simba akitokea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, lakini bado hajaonyesha maajabu ila kuna staa mkongwe, Ersto Nyoni ameshindwa kuvumilia na kusema jamaa ana kitu mguuni.
Nyoni aliyewahi kuitumikia Simba, Azam na Namungo, amesema ili Msimbazi ifaidike na kiwango cha kiungo mshambuliaji huyo Msauzi , inapaswa kumpa muda wa kuzoeana na wenzake pamoja na mazingira na huenda akaja kuwa msaada mkubwa wa kuzalisha mabao katika kikosi hicho.
Nyota huyo wa kimataifa wa zamani wa Tanzania aliyewahi kucheza soka la kulipwa Burundi katika klabu ya Vital’O aliliambia Mwanaspotu, alimtazama Maema katika mechi za CHAN na hata katika baadhi ya mechi akiwa na Mamelodi, aligundua ni mchezaji anayetumia akili kubwa anapokuwa na mpira.
“Huwezi kulinganisha uchezaji wa Maema akiwa timu ya Taifa na Mamelodi, zina mifumo tofauti na Simba, hivyo huwezi kulinganisha namna alivyokuwa anacheza kula na hapa nchini, kuna ugeni wa mazingira na anatakiwa kuzoeana na wachezaji wenzake,” alisema Nyoni na kuongeza;
“Maema ana akili kubwa ya kimpira, hilo haliwezi kuonekana kwa uharaka hadi atakapopata mechi nyingi, kama ilivyokuwa kwa Ellie Mpanzu wakati anaanza wengi walimuona kama hana kitu, ila wimbo huo umebadilika, timu nyingi zinatamani huduma yake.”
Nyoni aliongeza; “Ninachowashauri viongozi wa Simba ina wachezaji wazuri, kikubwa watulie wasiwape presha, naamini wakizoeana wanaweza wakawa hatari dhidi ya timu pinzani katika msimu huu.”
Nyoni aliyesifika kwa kumudu zaidi ya nafasi moja uwanjani kwa ufasaha kwa sasa hana timu baada ya kupewa ‘thank you ‘ na Namungo, japo amefichua katika dirisha dogo anaweza kuibuka katika moja ya klabu aliyomalizana nao hivi karibuni.