Samia aahidi neema kwa wakulima

Mbinga. Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa, endapo atapata ridhaa ya kuongoza miaka mingine mitano Serikali itafanya jitihada za kuimarisha masoko ya mazao na kuendelea kutafuta bei bora ili mkulima afaidike na nguvu zake.

Samia ametoa ahadi hiyo leo Septemba 21, 2025 wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma.

Amesema anatambua wilaya hiyo inafanya vizuri katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara, hivyo Serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa kuhakikisha wakulima wananufaika na jasho lao.

“Nafahamu Mbinga ni kituo kizuri na muhimu kwa uzalishaji wa mazao, tunataka kuhakikisha shughuli hii kubwa mnayofanya mnanufaika nayo, ahadi yangu kwenu ni kuhakikisha tunaimarisha masoko na kupata bei bora.

“Kingine tutendelea kutoa ruzuku ya pembejeo na mbolea na muhimu zaidi tutatoa huduma za ugaini, tutakuwa na BBT ya ugani, tutawatumia vijana walio na taaluma ya ugani kutoa huduma hizo, lengo hapa ni kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri zaidi upande huo,”amesema.

Kwa upande wa miundombinu, amesema Serikali itaendeleza ujenzi wa barabara kadhaa za wilaya hiyo katika viwango mbalimbali vitakavyoruhusu kupitika kwa mwaka mzima.

Katika eneo hilo pia ameahidi kujenga Daraja la Mto Lumeme na kuunganisha na barabara zake.

“Niwaambie ndugu zangu, hakuna mradi ghali kama barabara kilomita moja gharama yake ni vituo viwili vya afya na ndiyo maana hatuendi kwa kasi sana. Ahadi yetu ni kuwatumikia, mkitupa ridhaa ya kufanya kazi tutakwenda kuinua utu wa Mtanzania, utu wa kila mmoja bila kujali dini wala kabila lake.”

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro amesema wananchi wameridhishwa na maendeleo yanayotokana na utekelezaji wa ilani ya 2020/2025.

“Kuyaendeleza hayo mazuri tunaomba mumpe tena mgombea wa CCM ridhaa ya miaka mitano ili akaendeleze kazi ya kutuletea maendeleo kwenye Taifa letu,” amesema Dk Migiro.

Mgombea ubunge wa Mbinga Vijijini, Judith Kapinga amesema watu wa Mbinga Vijijini walikuwa wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 50 kufuata huduma za afya, lakini sasa kuna hospitali ya wilaya na vituo vipya vya afya vimejengwa pamoja na zahanati 17.

Akizungumzia pia namna kahawa ilivyokuza uchumi wa wakazi wa Mbinga Vijijini, amesema miaka mitano iliyopita kilo moja ya kahawa iliuzwa Sh3,600 lakini sasa bei imefikia Sh11,800 hadi Sh12,100.

“Sisi watu wa Mbiga Vijijini hatukuzoea kuyaona haya maendeleo yamekuwa kwa kasi sana, tumejengewa shule za msingi na sekondari pamoja na mabweni na nyumba za walimu. Kwa mambo haya mazuri hatuna cha kufanya zaidi ya kutiki itakapofika Oktoba 29.

“Ukija kwenye eneo la umeme zaidi ya vitongoji 300 vya Mbinga Vijijini vina nishati ya umeme, hatuna mashaka, upande wa barabara Tarura peke yake kwa kipindi cha miaka minne tumepewa bilioni 15,” amesema Judith.

Kwa upande wake mgombea ubunge wa  Mbinga Mjini, Jonas Mbunda amesema wananchi wa jimbo hilo  wameguswa na upatikanaji wa maji ikiwa ni matokeo ya kuboresha miundombinu ya maji iliyogharimu Sh14 bilioni.

“Hatuna cha kusema katika eneo hili la maji, hata hivi karibuni kulipokuwa na upungufu tumepewa tena Sh4.6 bilioni ambazo zimetumika kuongeza vyanzo vya maji. Vijiji vyote 78 vya Mbinga Mjini vina umeme, upatikanaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa kahawa umeongezeka hatuna cha kukulipa zaidi ya kuhakikisha unapata ushindi wa kishindo,”amesema Mbunda.

Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Ruvuma, Odo Mwisho  amesema amejipanga kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo akiahidi mkoa huo utaongoza kwa kupata kura nyingi za mgombea wa urais.

Mratibu wa Kanda ya Kusini na Mjumbe wa Kamati Kuu, Laila Ngozi amesema wananchi wana imani kubwa na wagombea wa CCM kwa kuwa, watasimamia kikamilifu yaliyoelekezwa katika ilani ya 2025/2030.